ACT Songwe kufikisha mahakamani msimamizi uchaguzi

Na Joachim Nyambo,Songwe. CHAMA cha ACT wazalendo mkoa wa Songwe kimesema kinatarajia kumpeleka Mahakamani Msimamizi wa Uchaguzi katika jimbo la Songwe kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wake kwenye uchaguzi wa mwaka huu baada ya kuenguliwa kwa mgombea wa ubunge kupitia chama hicho Michael Nyilawila na mgombea wa udiwani kata ya Kapalala,Bonifasi Thomas. Chama hicho pia kimesema hakijaridhishwa na hatua ya Mgombea wa ubunge kupitia Cha Mapinduzi(CCM) Filipo Mulugo kutangazwa na Tume ya Uchaguzi kupita bila kupingwa kikisema upo usanii mwingi uliofanyika kuwakandamiza waagombea waliochukua fomu kupitia ACT na Chadema. Akizungumza na mwandishi wa habari hizi,Katibu mwenezi na mawasiliano wa ACT wazalendo mkoa wa Songwe,Michael Nyilawila ambaye pia ndiye aliyegombea Ubunge na baadaye jina lake kuenguliwa alisema katri ya kasoro zilizobainika ni pamoja na Msimamizi wa uchaguzi jimbo la Songwe kubatilisha namba za wadhamini ili idadi ya wadhamini upungue isifikie 25 wakati yeye aliwapata 31. “Kati ya wadhamini 31 niliowapata kutoka kata mbalimbali walikatwa tisa wakabakia 22 na hapo wakatengeneza kesi ya kukosa kigezo kwakuwa sikufikisha wadhamini wasiopunga 25 kama maelekezo ya tume yalivyotaka.Na hii ilifanyika pia kwa mgombea wetu wa udiwani kata ya Kapalala.” “Lakini pia Msimamizi wa uchaguzi jimbo la Songwe alikataa kupokea kuturudishia fomu namba nane ya wadhamini na namba 10 ya tamko la kiapo.Tulipozihitaji tuliambiwa twende saa kumi ndipo tukachukue tunakwenda tunakuta wamebandika jina la mtu mmoja tayari kuwa amepita bila kupingwa.” “Kama vile haitoshi nilijaza fomu za kuweka pingamizi dhidi ya mgombea wa CCM na fomu ya kukata rufaa tarehe 26 mwezi wa nane saa tatu asubuhi niliziwasilisha ofisini kwa msimamizi wa uchaguzi lakini hakuwepo wakati maelekezo ilikuwa muda huo awepo ofisni kwaajili ya kutusikiliza nilikaa mpaka badae na kwakuwa alikuwa hapokei simu nikalazimika kuziacha kwa karani wake sambamba na barua ya malalamiko.” Nyilawila alisema jambo la kusikitisha ni kuona kuwa fomu hizo hazikuwasilishwa NEC makao makuu kulikotakiwa kwenda kufanyiwa rufaa za malalamiko ili haki iweze kutendeka na badala yake zilibakia ofisini kwa msimamizi. Alisema hata baada ya yeye na mwanasheria wa chama kufuatilia makao makuu ya NEC walibaini fomu zao kutowasilishwa hatua iliyoifanya tume kuona hakukuwa na mgombea wa vyama vingine aliyekuwa na vigezo zaidi ya Yule wa CCM na hivyo kumpitisha bila kupingwa. “Waliacha ofisi wazi katika masaa ambayo tulipaswa kuwasilisha mapingamizi wakajifanya wamekwenda kufanya kazi nyingine wakati tulikubaliana kabisa.Malalamiko yetu hawakuyawasilisha NEC tumefuatilia na kujiridhisha.Na huu ni mchezo ambao umekuwa ukifanyika katika chaguzi nyingi jimboni kwetu.Kwakuwa maelekezo yanatutaka kwenda mahakamani baada ya uchaguzi tutakwenda Mahakama ya rufaa kanda.Wanachi wako tayari kutuchangia fedha kwaajili ya kugharamia kesi ili tukapate haki yetu.” Alisisitiza Nyilawila. Akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya simu,msimamizi wa uchaguzi jimbo la Songwe Fauzia Hamidu pamoja na kusema hayupo tayari kuhojiwa na wanahabari kutokana na matatizo ya kiafya,alisema anachotambua yeye ni kuwa wagombea wa ubunge kupitia vyama vingine jimboni humo walikosa vigezo na ndiyo sababu akapitishwa wa CCM.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post