UTEKELEZAJI wa maamuzi yanayotolewa na Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) ni mdogo sana kutokana na nchi nyingi wanachama kutokuwa na utashi wa kisiasa, imeelezwa
Hukumu hizo hutolewa na Mahakama hiyo yenye makao makuu yake jijini hapa kutokana na malalamiko ya uvunjwaji wa haki za binadamu yaayowasilishwa na wadau mbalimbali kutoka nchi za Kiafrika.Hatua hiyo ni sawa na kuipuuza Mahakama hiyo
Kati ya nchi 30 zilizoridhia kuanzishwa kwa mahakama hiyo na nyingine nane zilizoruhusu watu binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali(NGO) kupeleka kesi mahakamani hapo ni Burkina Faso tu iliyotekeleza kwa asilimia 100 hukumu iliyotolewa na Mahakama hiyo.
“Hadi sasa ni Burkina Faso tu ndiyo iliyotekeleza kwa asilimia 100 hukumu mbili zilizotolewa na Mahakama hiyo lakini nchi nyinginezo ikiwamo Tanzania,bado,” alisisitiza Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Nouhou Diallo alipokuwa akijibu maswali kuhusu hali ya utekelezaji wa maamuzi ya mahakama hiyo mapema leo.
Naibu Msajili huyo alitoa ufafanuzi hu katika ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wanasheria walio katika leja ya mahakama hiyo ya kuwasaidia wananchi wa Afrika wanaohitaji huduma za mahakama.Mafunzo hayo ya siku tatu yaliyoanza leo yanashirikisha wanasheria kutoka nchi za Kiafrika.
Hata hivyo, Makamu wa Rais wa Mahakama hiyo, Jaji Ben Kioko alifafanua kuwa ingawa Kenya iliunda Kamati Maalum ya kushughulikia utekelezaji wa hukumu hiyo iliyotolewa Mei 26 mwaka 2017, hadi sasa kamati hiyo haijatoa taarifa yoyote.
Kwa mujibu wa taarifa za Mashirika yanayopigania haki za jamii za watu wanaoishi maisha ya asili (Indigenous people) kama Ogiek, zinasema Kamati hiyo, iliyoundwa bila kushirikisha hata mwakilishi mmoja wa jamii hiyo, ilishindwa kutekeleza majukumu yake kutokana na kukosa fedha na kusambaratika baada ya muda wake kwisha.
Katika hukumu yake, Mahakama ya Afrika ilisema kuwa, hatua ya serikali ya Kenya ya kuwafukuza watu wa jamii hiyo katika maeneo yao ya asili ya msitu wa Mau,kwa kisingizio cha kutunza misitu hiyo ni ukiukwaji wa haki za binadamu.Jaji Kioko pia alitoa mfano wa kesi ya Tanzania kuruhusu kuwa na mgombea binafsi katika nafasi za uchaguzi ambayo ilifunguliwa na Mchungaji Christopher Mtikila ambako Mahakama hiyo ilikubaliana na hoja za Mtikila ambaye sasa ni marehemu kuwa ni mfano wa hukumu ambazo hazijatekelezwa hadi sasa.
“Ingawa Bunge Maalum la Katiba la Tanzania lilipitisha kuwa na mgombea binafsi lakini najua kuwa mchakato wa Katiba mpya Tanzania bado haujakamilika hivyo utekelezaji wa hukumu hiyo nao haujafanyika hadi sasa,” alieleza Jaji Kioko
Mapema akifungua mafunzo hayo,Rais wa Mahakama hiyo,Jaji Sylvain Ore alisema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia wanasheria hao kutoa huduma bora kwa wateja wao ambao ni wananchi wa Afrika wanaopeleka kesi zao katika mahakama hiyo.
Tangu kukubaliwa kwa itifaki ya kuanzishwa kwa mahakama hiyo mwaka 1998,ni nchi 30 tu katika ya 54 wanachama wa Umoja wa Afrika(AU) ndizo zilizoridhia itifaki hiyo.
Hata hivyo,kati ya nchi hizo 30,ni nchi nane tu ambazo zimetoa tamko (Declaration) la kukubali kuruhusu watu binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali(NGO) kupeleka moja kwa moja kesi zao mahakamani hapo.
Bila ya tamko hilo Mahakama hiyo haitakuwa na mamlaka ya kushughulikia kesi zinazofikishwa mbele yake na watu binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali.
Nchi zilizotoa tamko hilo ni Benin,Burkina Faso, Ivory Coast, Ghana,Malawi,Mali, Tunisia na Tanzania.
Tanzania ndio nchi inayoongoza kwa wananchi wake kufungua kesi nyingi dhidi ya Serikali yao katika Mahakama hiyo
Kati ya kesi 178 zilizofunguliwa Mahakamani hapo tangu ilipohamia Arusha mwaka 2007, nusu ya kesi hizo zimefunguliwa na Watanzania dhidi ya Serikali yao kwa madai mbalimbali ya ukiukwaji wa haki za binadamu hasa baada ya kesi nyingi kutolewa hukumu na Mahakama za ndani.
ReplyForward |