Na Esther Macha - Malunde 1 blog Songwe
MAHAKAMA kuu ya Tanzania kanda ya Mbeya
imemhukumu ,Amanirabi Kalinga (19) mkazi wa kijiji cha Mpanda
wilayani Mbozi mkoani Songwe kunyongwa hadi kufa baada ya kukutwa na
hatia ya kuua kwa kukusudia kinyume na kifungu cha sheria 196 kanuni ya
adhabu sura ya 16 marekebisho ya sheria mwaka 2002.
Akitoa hukumu hiyo jana,jaji wa mahakama
kuu kanda ya mbeyaDkt,Adam Mambi alisema mahakama imetoa hukumu hiyo
kutokana na kuridhishwa na ushahidi wa upande wa mashitaka ambapo
alisema adhabu hiyo iwe fundisho kwa vijana wengine wenye tabia za
kujichukulia sheria mkononi.
Awali akisoma shauri hilo mahakamani
hapo Jaji Mambi alisema mshitakiwa anakabiliwa na kesi ya kumuua na
kisha kukata sehemu za siri za Heron Kalinga kisha viungo kupeleka kwa
mganga wa kienyeji,mshitakiwa anakabiliwa na kesi namba 57 ya mwaka
2017.
Aidha Jaji Mambi aliongeza kuwa
mshitakiwa alimkuta marehemu na wenzake wakichunga ng’ombe na kumchukua
na kumpeleka kichakani na kumuua na kumtupa huku Joseph Mwashilindi
akishuhudia, Heron Kalinga akiangushwa chini na kumchoma kisu ambapo
baada ya tukio mshitakiwa alirudisha ng’ombe nyumbani kwa kina Heron
Kalinga.
Alisema baada ya kufika nyumbani kwa
marehemu alidai kuwa amewakuta wamepotea na baada ya kubanwa alienda
kuonyesha mwili ulipo huku sehemu za siri za marehemu akiwa zimekatwa na
alizipeleka kwa mganga wa kienyeji aliyejulikana kwa jina la Makamu
ambaye alihitaji viungo hivyo ili amfanyie dawa,(Ndagu).
Alisema kutokana na ushahidi uliotolewa
mahakamani hapo pasipo kuacha shaka,Kijana huyo atatumikia adhabu ya
kunyongwa hadi kufa ili iwefundisho kwa vijana wengine wenye tabia kama
hizo.
Naye wakili wa Serikali, Shindani
Michael alishukuru mahakama hiyo kwa kutenda haki kwa hukumu hiyo ili
iwe fundisho kwa wananchi wengine wenye nia ya kufanya makosa kama hayo
ya kutaka kujipatia mali kwa kudhuru wengine.
Nje ya Mahakama,mamia ya watu waliofika
mahakamani hapo kushuhudia hukumu hiyo,wakiongozwa na Yerode Samwel
mkazi wa Mbozi,walisema mahakama hiyo imetenda haki kwa kuwa matukio
hayo ya watu kuua wenzao ili wajipatie mali yamezidi kushika kasi.
Alisema hiyo itakuwa fundisho kwa
wengine kwani vitendo vya baadhi ya watu kutaka utajili kwa kuua wenzao
na kuchukua viungo kwa ajili ya kupeleka kwa waganga wa kienyeji
vimekuwa vikijitokeza bila kujali kuwa ni kosa kisheria na ni dhambi
mbele za Mungu.