Mamlaka
ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) nchini Tanzania
imetangaza bei za kikomo kwa bidhaa za mafuta nchini humo zitakazoanza
kutumika kuanzia leo Jumatano Septemba 4,2019.
Taarifa
iliyotolewa Jumanne Septemba 3,2019 kwa vyombo vya habari na mkuu wa
kitengo wa mawasiliano na uhusiano kwa umma wa Ewura, Wilfred Mwakalosi
amesema bei za jumla na rejareja za mafuta za petroli dizeli na mafuta
ya taa zimeongezeka.
Mwakalosi
amesema mafuta hayo ni yale yaliyoingia kupitia bandari ya Dar es
Salaam ambayo yameongezeka ukilinganisha na mwezi uliopita.
“Mwezi
huu (Septemba) bei za rejareja za petroli, dizeli na mafuta ya taa
zimeongezeka kwa Sh83 kwa lita (sawa na asilimia 3.87), Sh61 kwa lita
(sawa na asilimia 2.90), Sh46 kwa lita (sawa na asilimia 2.22),” amesema
Amesema
bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya petroli, dizeli na yanayoingizwa
kupitia bandari ya Tanga yameongezeka ikilinganishwa na toleo la mwezi
uliopita.
“Kwa
mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara mwezi huu bei
zimeongezeka kwa Sh108 kwa lita sawa na asilimia 4.95 na Sh72 (sawa na
asilimia 3,36),” amesema Mwakalosi.
Katika
taarifa hiyo, Mwakalosi amesisitiza bei ya mafuta ya taa kwa mikoa ya
kaskazini zitaendelea kutumika zile zilizochapishwa mwezi uliopita kwa
sababu hakuna shehena ya bidhaa hiyo iliyoingia kupitia bandari ya
Tanga.