Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Mbunge wa Mtama Nape
Nnauye aliyefika Ikulu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kumuomba
msamaha Rais Dkt. Magufuli kufuatia tukio lililotokea miezi iliyopita.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe
Magufuli akifurahia jambo pamoja na Mbunge wa Mtama Nape Nnauye
aliyefika Ikulu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuomba msamaha mara
baada ya kuzungumza na wanahabari.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Mbunge wa Mtama Nape
Nnauye mara baada ya mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam.Na Herieth Makwetta, Mwananchi
Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema amemsamehe mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye huku akielezea namna ambavyo mbunge huyo amekuwa akimuomba radhi.
Akizungumza Ikulu leo Jumanne Septemba 10, 2019 Rais Magufuli amesema kwa muda mrefu Nape amekuwa akimuomba msamaha kupitia ujumbe mfupi wa simu ya mkononi na kuwatumia baadhi ya wazee wa chama hicho tawala.
Rais Magufuli amesema Nape alifikia hatua ya kwenda kwa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula, mjane wa Baba wa Taifa, Maria Nyerere pamoja na Mkurugenzi Mkuu mstaafu wa Idara ya Usalama wa Taifa nchini Tanzania, Apson Mwang'onda
“Alienda kwa mzee Mangula, amefika mpaka kwa Mzee Apson, Mama Nyerere amehangaika kweli lakini baadaye ni katika hiyohiyo sisi tumeumbwa kusamehe.”
“Leo nimemuona asubuhi amekuja hapa baadaye nikaona siwezi nikamzuia, ngoja niache shughuli zangu nimuone nilikuwa na kikao kingine kikubwa anachozungumza ninaomba baba unisamehe,” amesema Magufuli.
Kiongozi mkuu huyo wa nchi amesema, “Na mimi nimeshamsamehe tena kwa dhati kutoka moyoni mwangu, nimeshamsamehe na nimeshamsamehe kweli. Nape nenda ukafanye kazi, Mungu akujalie.”
“Unamuona kabisa huyu mtu anaomba msamaha na leo kaniomba aje anione na saa nyingine wasaidizi wangu wamekuwa wakipata hizo habari,” amesema Rais Magufuli
Awali, akizungumza Nape aliyewahi kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM amesema, “nimekuja kumuona (Magufuli) kama baba yangu, lakini mwenyekiti wa chama changu, Rais wangu kwa sababu wote mnajua mambo yaliyopita yalitokea ni mengi hapa katikati na mimi kama mtoto wa CCM mwanaye niliona ni vizuri nije niongee na baba yangu.”
“Kwa hiyo baada ya kupata fursa nimekuja nimemuona na mle ambamo nilimkosea kama baba yangu nimeongea naye na baba amenielewa, ameniambia amenisamehe na amenipa ushauri ambao nitaufanyia kazi na naamini baada ya hapa mambo yatakwenda vizuri.”
Mbunge huyo amesema, “kwa kweli kwa dhati ya moyo wangu nimshukuru sana sana, amenipa fursa kubwa, ndefu na ameongea maneno mengi kwangu na ushauri wake nimeuchukua.”
Ingawa si Nape wala Rais Magufuli waliozungumza hasa kwa nini wamekutana lakini katika siku za hivi karibuni kuliibuka sauti za viongozi mbalimbali wakiwamo za wabunge wa CCM, January Makamba (Bumbuli) na Willium Ngeleja (Sengerema) wakizungumzia suala la waraka ulioandika na makatibu wakuu wa CCM waliopita, Yusuf Makamba na Abdurahman Kinana.
Wazee hao wa CCM waliandika waraka huo kulalamikia mambo mbalimbali kwenda kwa Katibu wa Baraza la ushauri wa viongozi wa CCM, Pius Msekwa wakizungumzia mmoja wa wanaharakati ambaye amekuwa akiwachafua bila hatua kuchukuliwa.
Mpaka sasa bado haijafahamika kama hatua zimechukuliwa na hivi karibuni, Rais Magufuli alisema January na Ngeleja walikwenda kumwomba radhi kuhusu sauti hizo alizodai kuwa ni za kwao.