Na Mwandishi Wetu, KIA
Serikali ya Tanzania imepokea Faru Tisa kutoka Mfuko wa Grumet (GF) nchini Afrika Kusini.
Faru
hao wamepokelewa alfajiri Saa 9 jana katika Uwanja wa ndege wa
Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), na kusafirishwa kwa ndege kuelekea
Ikolongo-Grumet iliyopo Hifadhi ya Serengeti.
Aidha
wakati Faru hao wakiwasili nchini, ilielezwa Faru mmoja alifariki akiwa
Afrika Kusini wakati wa harakati za kuwasafirisha kuja nchini.
Hafla
ya kuwapokea Faru hao ilihudhuriwa na viongozi mbalimabli wa Serikali
wakiwamo Wakuu wa Mikoa ya Kilimanjaro Anna Mghwira na Mkuu wa Mkoa wa
Arusha Mrisho Gambo, Makamishna wa Uhifadhi wa Taasisi za TANAPA, TFS,
NCAA na TAWA, Wenyeviti wa Bodi wa mashirika hayo na viongozi wengine.
Akizungumza
wakati wa hafla ya makabidhiano kati ya serikali na Mfuko wa Grumet,
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Costantine Kanyasu alisema, serikali
itahakikisha inawalinda wanyama hao kwa gharama yeyote.
“Faru hawa tutawalinda kwa gharama zozote iwe za kisanyansi au kienyeji,” alisema Naibu Waziri Kanyasu.
Kwa
upande Kamishna Uhifadhi Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA),
Dk. James Wakibara alisema wanyama hao walikuwapo muda mrefu
“Kutoweka
kwao ni kwasababu ya matatizo ya ujangiri, baada ya juhudi kubwa
zinazofanywa na Wizara ya Maliasili hatua inayofuatana sasa ni kuanza
kuwarudisha,” alisema Dk. Wakibara.
Kamishna
Uhifadhi wa Hifadhi za Taifa Tanzania TANAPA Dk. Allan Kijazi alisema
wamefarijika kupata Faru watakaoongeza idadi kwenye mfumo wa Ikolojia ya
Serengeti.
Naye
Kamishna Uhifadhi Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Dk. Fredy
Manongi alisema kwa miaka mingi idadi ya Faru ilikuwa ikishuka Tanzania
kwa hivyo mkakati uliowekwa mwaka huu ni kuongeza idadi ya Faru.
“Tunaamini mkakati wetu utafanikiwa kwa sababu nia ni kuongeza idadi ya Faru nchini,” alisema Dk. Manongi.
Mwisho.
Kamishna Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa TANAPA Dk.Allan Kijazi akizungumzia ujio wa Faru hao nchini Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA). |