Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mheshimiwa Xi Jinping, leo asubuhi tarehe 29 Septemba 2019 amemtunukia Waziri Mkuu Mstaafu Mheshimiwa. Dk. Salim Ahmed Salim, Nishani ya Juu ya Urafiki ya Jamhuri ya Watu wa China ikiwa ni sehemu ya matukio ya maadhimisho ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China iliyofanyika jijini Beijing. Mheshimiwa Dkt. Salim anakuwa mwafrika wa kwanza kupewa heshima na tuzo hiyo ya juu katika historia ya China.
Nishani hiyo ilipokelewa na Bi. Maryam Salim, Binti ya Dk. Salim Ahmed
Salim ambaye pia ni Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Albania
kwa niaba ya Baba yake kutokana na kushindwa kuhudhuria kwa sababu za
kiafya. Katika tukio hilo, Serikali ya Tanzania iliwakilisha na Balozi
wa Tanzania nchini China Mheshimiwa Mbelwa Kairuki.
Hafla hiyo kubwa ya kitaifa ya kukabidhi nishani ilihudhuriwa na
viongozi waandamizi wa Chama na Serikali ya China akiwemo Makamu wa Rais
Mheshimiwa Wang Qishan, Waziri Mkuu Mheshimiwa Li Keqiang, Spika wa
Bunge Mheshimiwa Li Zhanshu na Wajumbe wote wa Kamati Kuu ya Chama cha
Kikomunisti cha China na Baraza la Taifa.
Mbali na Dk.Salim, wengine waliotunukiwa Nishani ya Urafiki ni pamoja
na Kiongozi wa Chama cha Kikoministi cha Cuba Jenerali Raul Castro, Dada
wa Mfalme wa Thailand Maha Chakri Sirindhorn, Kiongozi wa Jumuiya ya
Urafiki ya China na Urusi Ndugu Galina Kulikova, Waziri Mkuu Mstaafu wa
Ufaransa Jean-Pierre Raffarin na Bi Isabel Crook kutoka Canada.
Vilevile Rais Xi alitoa Nishani ya Jamhuri na Nishani ya Heshima ya
Taifa kwa raia 36 wa China kwa kutambua mchango wao mkubwa katika
maendeleo ya Taifa la China kupitia kazi zao katika fani mbalimbali.
Nishani ya Juu ya Urafiki ya Taifa la China imetolewa kwa Dkt. Salim
kutokana na mchango wake wa kuiwezesha Jamhuri ya Watu wa China kuwa
Mwanachama wa Umoja wa Mataifa mwaka 1971 alipokuwa Mwakilishi wa Kudumu
wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa. Aidha, mchango wa Dk. Salim
katika kuimarisha mahusiano kati ya China na Tanzania wakati
aliposhikilia nyadhifa mbalimbali umetajwa kama sababu ya kutunukiwa
Nishani hiyo. Vilevile, mchango wa Dk.Salim katika kujenga mahusiano
kati ya China na Afrika akiwa na nafasi ya Katibu Mkuu wa OAU umetajwa
kuwa sababu nyingine ya kutunukiwa Nishani.
Tukio la Kutoa Nishani limetangazwa moja kwa moja na Televisheni zote za
Jamhuri ya Watu wa China na kushuhudiwa na watu zaidi ya Milioni 500.
Kwa mujibu wa maelezo ya Balozi wa Tanzania nchini China Ndugu Mbelwa
Kairuki Kupitia tukio la leo, mamilioni ya Wachina hususan vijana
wamepata fursa ya kufahamu nafasi na mchango wa Tanzania na Bara la
Afrika katika historia ya taifa lao. Aidha, tukio la leo limeifanya
Tanzania kufahamika kwa watu wengi zaidi nchini China kupitia tukio mara
moja. Hatua hiyo itaamsha udadisi na hamasa miongoni mwa Wachina wengi
wa kizazi kipya kutaka kuifahamu zaidi Tanzania. Hali hii yaweza
kujitafsiri katika fursa kubwa ya kukua kwa utalii, biashara na
wawekezaji ikizingatiwa kuwa wananchi wa China hutoa mwitikio mkubwa
kwa nchi ambazo husemwa vizuri na kuthaminiwa na Serikali yao.
Aidha Balozi Kairuki ameeleza kwamba maadhimisho ya miaka 70 ya Jamhuri
ya Watu wa China mwaka huu yanaambatana na maadhimisho ya miaka 55 ya
urafiki na udugu kati ya China na Tanzania kufuatia kuanzishwa kwa
mahusiano rasmi ya kidiplomasia mwaka 1964. Uhusiano wa China na
Tanzania uliotokana na uhusiano mzuri wa waasisi wa mataifa haya mawili,
Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Mao
Tsetung. Uhusiano huo umeendelezwa na viongozi wa pande zote mbili ambao
umekuwa ukiimarika siku hadi siku. Uhusiano huu umekwenda mbali zaidi
ya uhusiano kati ya Serikali na Serikali na kushamiri kwa uhusiano wa
watu kwa watu.
Ni kwasababu hiyo, katika maadhimisho ya miaka 70 ya Taifa la China,
Jumuiya ya Urafiki wa watu wa China na Tanzania ni miongoni mwa Jumuiya
za mataifa 17 yenye urafiki wa majira yote na China walioalikwa
kushiriki kwenye maadhimisho hayo na tarehe 1 Oktoba 2019 watakuwa na
gwaride lao maalum. Katika jumuiya hizo 17, Kutoka Barani Afrika ni
Tanzania na Zambia ndio watahudhuria.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,