Makubaliano
hayo yalifanyika Jijini Dar es Salaam jana (Septemba 19, 2019) ambapo
serikali ya Tanzania iliwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi ili hali Poland
iliwakilishwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Marcin Przydacz.
Akiongea
na waandishi wa habari mara baada ya makubaliano hayo, Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi
amesema kuwa lengo la makubaliano hayo ni kukuza ushirikiano uliopo kati
ya nchi hizi.
"Kwa
sasa, tunashirikiana na Poland katika maeneo kadhaa ikiwa ni pamoja na
biashara ambayo takwimu zinaonesha kwamba biashara kati ya Tanzania na
Poland zimepanda kutoka milioni 77.7 mwaka 2016 mpaka milioni 124.5
mwaka 2017. Bidhaa za Tanzania zinazouzwa Poland ni pamoja na chai,
kahawa na tumbaku. Tanzania inanunua Poland bidhaa mbalimbali kama tairi
za magari, vifaa vya maabara na vifaa vya umeme," alisema Prof.
Kabudi
Prof.
Kabudi aliongeza kuwa, fursa za biashara baina ya nchi hizi mbili bado
ni nyingi na imekubaliwa kuwa balozi zetu na taasisi zingine za Serikali
zetu zitumike kuongeza ushirikiano katika biashara. "Kwa hili,
tunawaomba wafanyabishara wetu kuchangamkia fursa mbalimbali za
biashara," Aliongeza Prof. Kabudi
Kwa
mujibu wa Waziri Kabudi, Tanzania na Poland zinashirikiana kwenye
miradi mikubwa miwili. Mradi wa kwanza ni wa kiwanda cha kuunganisha
trekta, kilichopo Kibaha ambao unatekelezwa kwa mkopo wa riba nafuu
kutoka Serikali ya Poland. Kupitia mradi huu, jumla ya trekta 2400
zinaunganishwa nchini kupitia kampuni ya URSUS ya Poland. Tayari trekta
875 zimeshaunganishwa. Mradi huu utaongeza uzalishaji kwenye sekta ya
kilimo na kuleta mapinduzi ya kilimo kutoka kutumia jembe la mkono
kwenda kutumia trekta.
Mradi
mwingine ni ule wa kujenga maghala ya kuhifadhia nafaka ambapo jumla ya
maghala 8 yanajengwa katika kanda zote zinazohifadhi chakula nchini.
Mradi huu utaongeza uwezo wa Serikali wa kuhifadhi nafaka kutoka tani
250,000 kwa sasa hadi tani 500,000.
Katika
hatua nyingine, tumekubaliana pia kutoa fursa ya elimu ambapo
watanzania sasa watapata fursa ya kwenda kusomaPoland ambapo fursa
nyingi zitatolewa katika fani ya udaktari wa aina mbalimbali, uhandisi,
sayansi, Tehama, kilimo na maeneo mengine.
Prof.
Kabudi aliongeza kuwa, Tanzania imeendelea kuvutia watalii kutoka nchi
ya Poland. Kila mwaka, watalii wapatao 12,000 wamekuwa wakitembelea
visiwa vya Zanzibar kwa ndege zinazotoka miji mbalimbali ya Poland moja
kwa moja mpaka Zanzibar. Idadi ya watalii inaendelea kuongezeka kutoka
watalii 12,241 mwaka 2017 hadi watalii 18, 853 mwaka 2018.
Kwa
upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland, Marcin Przydacz
amesema kuwa Serikali yake itaendelea kuwahimiza Wapoland kuja kuwekeza
nchini kwa wingi na hasa kwenye maeneo ya uzalishaji wa dawa, kilimo
hususan katika uongezaji wa thamani ya mazao ya kilimo, uzalishaji wa
mashine za viwandani na uzalishaji wa bidhaa za viwandani.
Pia,
Waziri Przydacz ameahidi kuwa Serikali yake itaendeleea kuunga mkono
juhudi za Serikali ya awamu ya tano inayooongozwa na Mhe. Rais Magufuli
ya kutafuta suluhisho la changamoto ya uhaba wa maji inayokabili
wananchi sehemu mbalimbali nchini.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Yokohama, Japan
19 Septemba, 2019