TAASISI YA USULUHISHI YAOMBA MABADILIKO YA SHERIA

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na wajumbe kutoka Taasisi ya Usuluhishi Tanzania walipofika kumtembele ofisini kwake jijini Dar es salaam
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe kutoka Taasisi ya Usuluhishi Tanzania walipofika kumtembele ofisini kwake jijini Dar es salaam.


Na Lydia Churi-Mahakama

Taasisi ya Usuluhishi Tanzania (The Tanzania Institute of Arbitrators) imeiomba Mahakama ya Tanzania kusaidia katika mchakato wa mabadiliko ya Sheria ya Usuluhishi ya mwaka 1931 (The Tanzania Arbitration Act, 1931) kwa kuwa sheria hiyo hivi sasa imepitwa na wakati. 

Sheria ya Usuluhishi ya mwaka 1931 ilifanyiwa marekebisho (Amendment) mara moja tangu Tanzania ipate Uhuru wake ambapo marekebisho hayo yalifanyika mwaka 1971. 

Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Gabriel Malata alitoa ombi hilo leo wakati ujumbe kutoka Taasisi hiyo ulipomtembelea Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ofisini kwake kwa lengo la kujenga mahusiano ya kiutendaji kati yake na Mahakama ya Tanzania na pia kutambulisha uongozi mpya wa Taasisi hiyo.

Akizungumzia mchakato wa mabadiliko ya Sheria ya Usuluhishi, Bwana Malata aliiomba Mahakama kuishirikisha Taasisi hiyo kwa karibu katika mchakato wa mabadiliko ya Sheria ya Usuluhishi na hususan katika hatua ya utengenezaji wa kanuni.

Alisema Taasisi ya Usuluhishi Tanzania iko tayari kutoa maoni na mapendekezo pindi hatua hiyo itakapofikiwa. Aliongeza kuwa hivi sasa Taasisi hiyo imejikita katika kutoa Elimu husika katika Shule ya Sheria (Law School of Tanzania) ambapo wanafanya vipindi ili waweze kupata Wasuluhishi bora hapo baadaye.

Mwenyekiti huyo alisema Taasisi yake inao mfumo unaowatambua Wasuluhishi hai na hivyo ameiomba Mahakama kuishirikisha ili wapatikane wasuluhishi hai. Sheria ya Tanzania inaruhusu kuteua Wasuluhishi.

Kwa Upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania amesema Mahakama iko tayari kurekebisha Kanuni za Usuluhishi pale inapobidi kufanya hivyo ili Tasnia ya usuluhishi ifanye kazi vizuri na kuwasaidia wananchi kwa haraka.

Alisema suala la usuluhishi ni muhimu kwa Mahakama ya Tanzania kwa kuwa litasaidia kupunguza idadi ya kesi mahakamani.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, utafiti unaonyesha kuwa suala la usuluhishi wa migogoro nje ya Mahakama linaweza kufanyika katika ngazi zote za Mahakama kuanzia Mahakama za Mwanzo mpaka Mahakama ya juu. 

Aidha, Jaji Mkuu ameishauri Taasisi ya Usuluhishi Tanzania kuhakikisha inatoa zaidi elimu juu ya masuala ya usuluhishi kwa kuwa wananchi wengi bado hawana uelewa wa masuala hayo.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post