Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Wazee na Watoto; Mh. Ummy Mwalimu na Afisa Mkuu wa Ukaguzi wa
Mahesabu ya Ndani wa Benki ya NMB, Juma Kimori wakiwa katika picha ya
pamoja na wenyeji wao kutoka hospitali za Muhimbili na Mloganzila.
Afisa Mkuu wa Ukaguzi wa Mahesabu
ya Ndani wa Benki ya NMB, Juma Kimori akimkabidhi Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto; Mh. Ummy Mwalimu masada wa vitanda
15 kwa ajili ya chumba cha watoto wagonjwa waliopo kwenye uangalizi
maalum(ICU) katika hospitali za Muhimbili na Mloganzila za jijini Dar es
Salaam.
Katika kutambua afya ni suala
muhimu sana kwa maendeleo ya jamii, Benki ya NMB imekabidhi vitanda 15
vyenye jumla ya thamani ya milioni 45 kwa ajili ya chumba cha watoto
wagonjwa waliopo kwenye uangalizi maalum (ICU) katika hospitali za
Muhimbili na Mloganzila za jijini Dar es Salaam.
Akikabidhi msaada huo kwa Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, Mkaguzi Mkuu
wa Mahesabu ya Ndani wa NMB, Juma Kimori, alibainisha kwamba thamani ya
vitanda vyote ni Sh. Milioni 45 huku akifafanua kuwa kitanda kimoja cha
ICU ya watoto kimegharimu Sh. Milioni 7.5 na kuahidi kuendelea
kushirikiana na serikali kuboresha sekta ya afya.
Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na
Ukunga katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Zuhura Mawona, aliishukuru
na kuipongeza NMB kwa msaada huo na kuiomba iendelee kutoa msaada zaidi
kwa ajili ya chumba hicho maalum kwa watoto.
“Tulipeleka maombi NMB na
wametujibu hatuchoki, tunaendelea kuwaomba mtushike tena mkono, maana
mahitaji ya vitanda katika chumba hicho muhimu cha kuokoa maisha ya
watoto ni mkubwa, bado tunahitaji vingine saba mkiguswa tena mtukumbuke.
“Kabla ya wodi hii kuanza watoto
walikuwa wanachanganywa kwenye ICU za wakubwa na kule vitanda sio sawa
na hivi tulivyopokea vya NMB hata sisi wahudumu hatupati tabu sana
kuvinyanyua wala mgonjwa haumii kila kitu kinasetiwa kwenye umeme
asanteni sana NMB,” alisema Mawona aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji
wa Hospitali ya Hospitali ya Taifa Muhimbili.