Na Peter Haule na Josephine Majura, WFM, Dodoma
Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji, ameiagiza Bodi ya
Manunuzi na Ugavi kuwachukulia hatua waliopelekwa kwenye baraza la
maadili kulingana na uzito wa makosa yao ili taaluma hiyo iendelee
kufanya kazi kwa weledi bila rushwa.
Agizo hilo limetolewa Jijini Dodoma wakati wa mkutano wa 10 wa Wataalamu wa Ununuzi na ugavi kutoka maeneo mbalibali nchini.
Dkt. Kijaji alisema kuwa, kuna ununuzi usiozingatia sheria na kanuni na
kusababisha kununua bidhaa zilizo chini ya kiwango, ununuzi hewa wa
huduma na bidhaa na kutokuwepo kwa kumbukumbu za ununuzi na mikataba
hewa licha ya uwepo wa wataalam hao.
“Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi wa Umma kwa mwaka 2018/19 inaonesha
mikataba 12 kutoka taasisi tisa za umma yenye thamani ya shilingi
bilioni 25.8 ina viashiria vya rushwa kwa kuwa utaratibu wa manunuzi kwa
mikataba hiyo haukufuatwa”, alieleza Dkt. Kijaji
Alisema kuwa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
inaonesha kuwa ununuzi wa jumla ya Sh. bilioni 16.6 haukuwa kwenye
bajeti wala mpango wa ununuzi ulioidhinishwa na Sh. bilioni 24.85
zimetumika kulipa mikataba ambayo haikuwa na hati ya utekelezaji.
Dkt. Kijaji amewataka waajiri wote kutoa ushirikiano kwa bodi za
kitaaluma hususan linapojitokeza suala la usimamizi wa maadili kwa
wataalamu waliosajiliwa na bodi husika, kwa kuwa hakuna ufanisi bila
maadili.
Aidha Dkt. Kijaji, ameupongeza uongozi wa PSPTB kwa hatua
zilizochukuliwa za kusimamia mahitaji ya ajira ya kada ya ununuzi na
ugavi kwa kuwapeleka mahakamani watu wanaofanya kazi za ununuzi na ugavi
bila kuwa na sifa stahiki.
Hivyo akawataka waajiri wote kuhakikisha wanaajiri watumishi wenye sifa
zinazotambuliwa na PSPTB na kuzingatia mahitaji yaliyopo kwenye waraka
wa Maendeleo ya utumishi wa mwaka 2015.
Naibu Waziri Dkt. Ashatu Kijaji, ameiagiza Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi
na Ugavi (PSPTB) kufanya tathmini ya uwezo na uadilifu wa taasisi za
umma zilizobeba dhamana ya ununuzi Serikalini.
Alielekeza kuwa taarifa ya Baraza la Maadili iwasilishwe wizarani mapema
ili iweze kupitiwa na kufanya maamuzi kwa kushirikiana na vyombo
vingine vya Serikali.
Amesema kuwa Wizara ya Fedha na Mipango itaendelea kuunga mkono juhudi
za Bodi zinazolenga kuondoa kabisa uzembe na ukiukwaji wa maadili katika
fani ya ununuzi na ugavi, kwa kuwa bajeti ya ununuzi wa Serikali ni
takribani asilimia 80 ya bajeti yote.
Kwa upande wake Kamishna wa Idara ya Sera ya Ununuzi wa Umma, Dkt.
Fredrick Mwakimbinga, alisema kuwa Bodi inafanya jitihada za dhati
kuhakikisha taaluma ya ununuzi na ugavi inatoa mchango unaotarajiwa
katika ujenzi wa uchumi wa viwanda kulingana na malengo ya Serikali ya
Awamu ya Tano, ili kutimiza malengo hayo bodi imetoa mafunzo mahususi
kwa taasisi mbalimbali ambayo yameongeza ufanisi katika taasisi husika.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB, Bw. Godfrey Mbanyi, amesema
kuwa Bodi hiyo imeahidi kufanyia kazi maagizo yote yaliyotolewa na Naibu
Waziri Dkt. Kijaji. Amebainisha kuwa licha ya kuwa na Sheria
inayowataka watumishi wanaofanya kazi ya ununuzi na ugavi kusajiliwa,
bado wapo ambao hawafanyi hivyo, Bodi itaendelea kuchukua hatua stahiki
kwa wale wote watakao kiuka sheria.