Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu imeuambia upande wa utetezi katika kesi ya
uhujumu uchumi inayomkabili Mwandishi wa Habari, Erick Kabendera kuwa
waende wenyewe kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) ili kujua hatma
ya barua ya Kabendera ya makubaliano ya kuomba msamaha na kukiri kosa.
Hatua
hiyo imefikiwa wakati kesi hiyo ilipoitwa Mahakamani hapo mbele ya
Hakimu Mkazi Mkuu, Janet Mtega kwa ajili ya kutajwa na kudaiwa kuwa
upelelezi bado haujakamilika hivyo upande wa utetezi wakawasilisha hoja
zao.
Wakili
wa Utetezi, Jebrah Kambole amesema Oktoba 11,2019 waliitaarifu Mahakama
juu ya Kabendera kuandika barua ya kuomba msahama na kukiri kosa kwenda
kwa DPP lakini mpaka leo ni miezi miwili hawajapata mrejesho wowote
kutoka kwa DPP na Mtuhumiwa bado yuko gerezani na ni mgonjwa.
Kufuatia
hoja hizo, Hakimu Mtega ameutaka upande wa utetezi waende wenyewe
kufuatilia jalada la kesi kwa DPP ili wajue kinachoendelea na
ameiahirisha kesi hiyo hadi itakapotajwa tena Desemba 18, mwaka huu.