NA SALVATORY NTANDU
Wachimbaji
na wamiliki wa maeneo yenye madini ya ujenzi wilayani kahama mkoani
Shinyanga wametakiwa kuwa leseni za uchimbaji ambazo zitawasaidia
kuepukana na kutaifishwa kwa madini hayo pindi yanapokamatwa na
kubainika kutolipiwa kodi ya serikali.
Kauli
hiyo imetolewa jana na Kamishina wa madini wa mkoa wa Shinyanga
Mhandisi Joseph Kumburu kwenye mkutano maalumu na wamiliki wa maeneo ya
uchimbaji, wachimbaji, wasafirishaji mjini kahama kuhusiana na kuwa na
leseni za uchimbaji wa madini ya Ujenzi.
Amesema
kwa mujibu wa sheria ya Madini ya mwaka 2010 kifungu cha sita na
marekebisho ya kifungu cha 30 ni kosa la kufanya shughuli za madini bila
kibali hivyo wanapaswa kuwa na leseni na hawatakubali kuendelea na
uchimbaji holela wa madini ya ujenzi katika mji wa kahama.
“Tumekuja
kutoa elimu kwa kundi hilo linalojihusisha na shughuli za madini ili
waitambue sheria hii na namna inavyofanya kazi endapo tukiacha uchimbaji
huu holela ukaendelea katika wilaya ya kahama maeneo mengi yatabaki
kuwa na mashimo”alisema Kumburu.
Naye
mwenyekiti wa Wachimbaji wa madini ya Ujenzi katika wilaya ya kahama
Martine Clemency amesema bado wanakabiliwa na changamoto nyingi katika
uchimbaji wa madini hayo kutokana na mrundikano wa tozo pindi
wanaposafirisha madini ya ujenzi.
“Msafirishaji
wa madini haya anatozwa kodi shilingi 2500 kwa kila gari na wakati
mwingine hutozwa zaidi ya mara mbili kutokana na kuwepo kwa mageti mengi
kabla ya kufikisha mzigo kwa mteja wake jambo ambalo limekuwa
likisababisha usumbufu kwa madereva wangu”alisema Martine.
Kwa
upande wake ofisa Mazingira wa halamshauri ya mji wa Kahama Johanes
Mwebesa amesema halamshauri ya mji imetenga maeneo ya uchimbaji wa
madini katika kata ya Ngogwa na wachimbaji wote wa madini ya Ujenzi
waliopo mjini watalazimika kwenda huko ili kuzuia uharibifu wa
mazingira.
“Tumefanya
tahimini na kujiridhisha kuwa maeneo ambayo tumeyatenga yanafaa
kwaajili ya shughuli hizo na muda si mrefu mtalazimika kwenda huko na
kuondoka hapa mjini kwaajili ya shughuli hizo za uchimbaji madini
Ujenzi”alisema Mwebesa.
Mkutano
huo umejumusha wachimbaji,wamiliki wa magari na madereva wapatao 100 na
madini ujenzi ambayo yanapaswa kulipiwa ushuru ni pamoja na
kokoto,mchanga na moramu.