Na Bakari Kiango, Mwananchi
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amekemea vitendo vya rushwa na
kuchafuana kwenye mitandao ya kijamii katika chaguzi za chama hicho.
Kiongozi huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ametoa kauli hiyo leo
Alhamisi Desemba 12, 2019 katika mkutano wa Baraza la Wanawake la chama
hicho (Bawacha). Katika mkutano huo utafanyika uchaguzi wa viongozi wa
baraza hilo.
Uchaguzi ndani ya chama hicho utahitimishwa Desemba 19, 2019
utakapofanyika uchaguzi wa katibu mkuu, naibu katibu wakuu Bara na
Zanzibar pamoja na wajumbe wa mkutano mkuu. Desemba 18, utafanyika
uchaguzi wa mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa Bara na Zanzibar.
Tayari Baraza la Vijana la chama hicho (Bavicha) na baraza la wazee yamepata viongozi wake.
Katika uchaguzi wa Bawacha, Halima Mdee anagombea peke yake nafasi ya
mwenyekiti. Wanaowania umakamu mwenyekiti Bara ni Hawa Mwaifunga, Aisha
Luja, Marceline Stanslaus na Mary Nyagabona, kwa upande wa Zanzibar ni
Mariam Salum Msabaha, Sharifa Suleiman na Zeud Mvano Abdulahi.
Katika hotuba yake leo Mbowe amesema, “nimesikia kuna harufu ya rushwa
katika uchaguzi huu. Leo unatafuta uongozi ndani Chadema kwa rushwa?
Hiki siyo chama nilichokijenga.”
"Fitina na kutukanana kwenye mitandao ya kijamii sio jambo zuri. Nakemea
jambo hili na tutawachukulia hatua wote watakaobanika kufanya vitendo
hivi, msivyokuwa waadilifu sasa mnachukua huku na kule halafu
mnawaambia tupo pamoja," amesema Mbowe.
Amewataka wagombea kupambana na kwa hoja huku akitoa wito wa wajumbe
wa mkutano huo kutowachagua viongozi kwa kigezo cha rushwa badala yake
wasikilize na kuwapima kulingana na sera zao wakati wa kujinadi.
"Bawacha tunaiamini na inafanya kazi nzuri lakini ina mdomo. Mtu yeyote
atakayejiingiza kwenye vitendo vya rushwa hakitakii mema chama hiki,
shiriki uchaguzi kwa haki na upendo. Leo kampeni za kina mama
zinafanywa na wanaume? Kuna maisha baada ya uchaguzi," amesema
mwenyekiti huyo