Mfungwa Merald Abraham, aliyekataa kurudi Uraiani
Mfungwa mmoja aliyejulikana kwa jina la Merald Abraham, amekataa kurejea
Uraiani baada ya kuachiwa kwa msamaha uliotolewa na Rais Magufuli kwa
madai ya kuwa hana pa kwenda na kutaka ahamishiwe katika Gereza la
Ukonga, Jijini Dar es Salaam.
Abraham ni miongoni mwa wafungwa 70 katika Gereza la Ruanda, waliopewa
msamaha Desemba 9, 2019, na jana Desemba 10 wakati wenzake wakiachiwa
huru, yeye alikataa kubaki huru hali iliyopelekea kujijeruhi usoni,
akishinikiza kuendelea kubaki mahabusu.
"Sina pa kwenda, bora nibaki Gerezani, ikiwezekana nitolewe hapa
nihamishiwe Gereza la Ukonga Dar es Salaam, ila sio Uraiani" amesema
Abraham.
Juzi wakati wa Maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanzania, ambayo
Kitaifa yalifanyika mkoani Mwanza, Rais Magufuli alitoa msamaha kwa
wafungwa takribani 5,533 na wafungwa 259 kati yao wanatoka mkoani Mbeya.