Na; Salvatory Cevin
Baada
ya kukithiri kwa matukio ya wanafunzi kupata mimba na uwepo wa ndoa za
watoto chini ya umri wa miaka 18 mkoani Shinyanga, hatimaye serikali
imeamua kutoa fomu maalum ambazo zitasaidia kuzihakiki ndoa zote
zinazotarajiwa kufungwa.
Hayo
yamebainishwa juzi na Ofisa maendeleo ya jamii wa mkoa wa Shinyanga,
Tedson Ngwale katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa
kijinsia kwa watoto na wanawake yaliyofanyika katika kijiji cha Penzi
kata ya Mondo wilayani Kahama yaliyofadhiliwa na shirika la World
Vision.
Amesema
katika mkoa wa Shinyanga kila halmashauri itapewa fomu hizo maalum
ambazo zitatumika kama mkataba wa kuhakiki ndoa zote katika maeneo yote
baada ya kubaini ndoa nyingi zinazofungwa ni za wanafunzi pamoja na
watoto chini ya umri wa miaka 18.
“Fomu
hizi zitahitaji mwoaji awasilishe nyaraka mbalimbali ili kutibitisha
umri wa anayekwenda kuolewa kama vile vyeti vya kuzaliwa kutokana na
kuwepo kwa ndoa batili za watoto ambazo zinafanyika kwa siri hususani
katika maeneo ya vijijini”alisema Ngwale.
Ngwale
amesema watendaji wa vijiji na kata watapaswa kufanya uhakiki huo kwa
kina kabla ya kuruhusu kufanyika kwa ndoa hizi kwa kutumia fomu hizo
ambazo zitakuwa na kiapo maalum ambacho kimtaka kuijaza kwa uaminifu na
uadilifu.
Mbali
na hilo, Ngwale amesema Serikali imeandaa mikataba maalum baina ya
wazazi wa wanafunzi baada ya kubaini wazazi mkoani humo kuwazuia watoto
wao wakike kufanya vizuri katika masomo yao ili waolewe jambo ambalo ni
kinyume na haki za watoto.
“Katika
mitihani ya mwisho hususani wa darasa la saba watoto wengi wakike
katika baadhi ya jamii mkoani humu wamekuwa wakizuiwa kufanya vizuri
,kupitia mikataba hii suala hili litakuwa limefikia mwisho kwani
mwanafunzi akibainika kufanya vibaya wazazi watakuwa wanachukuliwa hatua
za kisheria”alisema Ngwale.
Kwa
upande wake Ofisa mradi wa ENRICH kutoka shirika la World vision,
Magreth Mambali amesema katika siku hizi 16 za kupinga ukatili wa
kijinsia wamebaini katika maeneo ya vijijini wanawake na watoto ndio
wahanga wa ukatili.
“Mila
na tamaduni za kabila la wasukumu bado ni kandamizi kwa wanawake
hususani watoto wakike kwani husababisha wengi wao kuolewa katika umri
mdogo na kukosa haki zao za msingi kama vile elimu”alisema Mambali.
Takwimu
za mimba kwa wanafunzi kwa mwaka 2018 katika mkoa wa shinyanga
zinaonesha wanafunzi 69 walipata mimba huku mwaka huu wa 2019 wanafunzi
waliopata mimba wakiwa ni 120.