Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imeliondoa jina la Sudan kwenye orodha yake nyeusi ya nchi zinazokiuka uhuru wa kuabudu
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani jana ililiondoa jina la Sudan kwenye orodha nyeusi ya nchi zinazokiuka uhuru wa kuabudu, kwa mtazamo wa Washington, na wakati huo huo ikatoa onyo kwa Nigeria, Cuba na Nicaragua.
Sudan ni nchi pekee ambayo jina lake limeondolewa kwenye orodha nyeusi inayotolewa kila mwaka na wizara ya mambo ya nje ya Marekani, kuhusiana na nchi ambazo kwa mtazamo wa Washington zinatia wasiwasi mkubwa kuhusu ukiukaji wa haki ya kuabudu
Wakati Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Sudan, Abdalla Hamdok alipofanya safari nchini Marekani hivi karibuni, alitaka nchi yake iondolewe kwenye orodha ya Washington ya nchi zinazofadhili ugaidi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo amedai kupitia taarifa kwamba, uhuru wa kuabudu ni kipaumbele katika serikali ya nchi hiyo.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani vile vile imeongeza majina ya nchi za Nigeria, Cuba na Nicaragua kwenye orodha ya nchi zilizo "chini ya uangalizi" na kutangaza kuwa, ikiwa hali ya mambo katika nchi hizo, katika mtazamo wa Washington, haitaboreka, nchi hizo zitajumuishwa kwenye orodha nyeusi ya nchi hiyo