Naibu
Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima
akizungumza kwenye mkutano wa 25 wa Mawaziri wa Nchi Wanachama wa
Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaondelea
Madrid nchini Hispania.
Naibu
Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima
(mwenye tai nyekundu) akifuatilia majadiliano katika mkutano wa 25 wa
Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu
Mabadiliko ya Tabianchi unaondelea Madrid nchini Hispania. Pembeni yake
ni Afisa Misitu Mkuu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt Freddy Manyika.
Naibu
Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima
(wa pili kulia) akijadiliana jambo na ni Afisa Misitu Mkuu Ofisi ya
Makamu wa Rais Dkt Freddy Manyika. Wengine pichani kuanzia kushoto ni
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa na Hifadhi ya Mazingira (NEMC) Dkt.
Samuel Gwamaka na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
(TMA) Dkt. Agnes Kijazi.
Na Dkt. Freddy Manyika, Madrid, Hispania.
Tanzania
imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka na za
pamoja kushughulikia suala la mabadiliko ya tabianchi na athari zake.
Hayo
yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mussa Sima
katika mkutano wa 25 wa Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja
wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaondelea Madrid nchini
Hispania.
Aliwataka
wajumbe wanaoshiriki katika mkutano huo kuendelea kuchukua hatua
mahsusi za kushughulikia changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
“Tunahitaji
kuendeleza kasi ya kushughulikia mabadiliko ya tabianchi kwa kubainisha
malengo mahususi ya kupunguza tatizo hilo kwa kuchukua hatua zote
muhimu zinazohitajika” Sima alisisitiza.
Aidha
ameeleza kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi tayari zimeathiri
Tanzania kupitia matukio makubwa ya hali ya hewa ikiwemo mvua nyingi na
kuongeza kwa joto ambavyo vinasababisha mafuriko na kusambaa kwa
magonjwa ambukizi, upotevu wa mali na maisha ya wanadamu na uharibifu wa
miundombinu ya barabara na madaraja katika maeneo mengi ya nchi.
Pia,
Naibu Waziri alibainisha kuwa, kwa mujibu wa taarifa za Mamlaka ya Hali
ya Hewa Tanzania (TMA), Oktaba mwaka huu imekuwa na mvua nyingi
ulikinganisha na kipindi kingine kama hicho kwa karibu muongo mmoja
uliopita na kuathiri sekta zote muhimu, kama vile kilimo, afya, uvuvi,
mifugo, maji na afya hivyo kuongeza kwa magonjwa yakiwemo dengue na
malaria.
Katika
hatua nyingine Naibu Waziri Sima alibainisha kuwa Serikali ya Tanzania
chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli, imekuwa ikichukua hatua thabiti
ambazo zinachangia katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na
ongezeko la gesijoto licha ya ukweli kuwa haikuchangia katika chanzo
cha tatizo hilo.
Aliuarifu
mkutano huo kuwa Tanzania imenunua rada mbili zitakazotumiwa na TMA kwa
lengo la kuongeza ufanisi wa utabiri hali ya hewa na majanga yatokanayo
na athari za mabadiliko ya tabianchi, inaendela kupanua na kujenga
mtandao wa barabara za mabasi ya mwendo wa haraka katika jiji la Dar es
Salaam; inajenga reli ya viwango vya kimataifa (SGR) na kujenga bwabwa
la Mwalimu Nyerere ambalo litazalisha kiasi cha 2115MW.
“Utekelezaji
wa miradi hii sio tu unachochea mandeleo ya taifa na ukuaji wa uchumi,
bali unachangia pia katika upunguzaji wa gesijoto ambazo zinasabaisha
ongezo la joto la dunia ambalo husabaisha mabadiliko ya tabianchi” Sima
aliongezea.
Pamoja
na hayo, Sima aliuarifu mkutano wa Madrid kuwa, Tanzania imedhamiria
kuendelea kuongeza maeneo yanayonyonya gesijoto na kutunza uoto wa asili
kwa kuwa na eneo la misitu lenye ekari takiriban milioni 48, kuendelea
kuongeza eneo ambalo limehifadhiwa kwa kuongeza idadi ya hifadhi za
taifa na kuendelea na kampeni ya upandaji miti nchi nzima.
Alitoa
wito kwa jumuiya ya kimataifa kuunga mkono jitihada za Tanzania katika
kushughulikia suala la mbadiliko ya tabainchi na kuziomba nchi
zilizoendelea kuongeza juhudi zaidi katika kushughulikia suala la
mabadiliko ya tabianchi kwa kutekeleza miradi na kutoa fedha na
teknolojia kwa ajili ya kushughulikia tataizo hili.
Ujumbe
wa Tanzania katika Mkutano huo wa 25 wa nchi Wanachama wa Umoja wa
Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaofanyika Madrid, Hispania
kuanzia Tarehe 2 hadi 13, Desemba 2019 unaongozwa na Naibu Waziri Ofisi
ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima na
unahudhuriwa na washiriki zaidi 20,000 kutoka serikali za kitaifa,
majimbo, majiji, na halmashauri, asasi za kiraia, sekta binafsi, jumuiya
ya wanafanya biashara ambao wamekusanyika kujadiliana kuhusu
utekelezaji wa mkataba wa Mabadiliko ya tabianchi na makubaliano ya
Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi.