Na Hellen Kwavava Dar es Salaam.
Uandikishwaji wa watoto kwa Shule za Awali na Msingi nchini umeongezeka kutoka asilimia 35 kwa mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 78 kwa mwaka 2017 na hiyo imetokana na kupatikana kwa elimu bure ambayo ni sera ya serikali ya awamu ya tano toka ilivyoingia madarakani.
Aidha shule moja kati ya nne ndiyo inatoa chakula kwa asilimia 90 kuanzia asubui hadi Mchana na hasa kwa upande wa mjini pekee.
Akizungumza wakati akizindua Ripoti ya saba ya uwezo katika tathimini ya kujifunza kusoma na kufanya hesabu Tanzania ya mwaka 2019 Mkurugenzi wa Twaweza nchini Aidan Eyakuze alisema kuwa ripoti hiyo ilijikita kuangalia namna ya uelewa kwa watoto kuanzia miaka 6 hadi 16 katika kusoma hasa kwa wakati huu ambao serikali imewekeza katika elimu kuanzia shule za msingi hadi sekondari.
Eyakuze alisema kuwa ripoti hiyo ilibaini kuwa ufaulu kwa upande wa hesabu na kingereza kwa watoto hao bado umekuwa mdogo sana jambo ambalo ameiomba serikali kutilia mkazo kati masomo hayo ili kuongeza chachu ya watoto hao kwa kuyapenda masomo hayo na kufaulu vizuri.
“Kwenye ripoti hii tumebaini mambo kadhaa hasa kutokana na serikali hii kuwa na sera ya kuondoa ada kwa shule za msingi hii imepelekea uandiskishwaji wa watoto kupanda lakini pia sera ya kupeleka rukuzu moja kwa moja mashuleni bila kupitia Halmashauri hasa kwa shule hizi iliyoanza kutekelezwa mwaka 2016 hii imetoa hamasa kubwa kwa shule kuhakikisha wanafunzi wana huzulia na kuandikishwa bila shida”,alisema
Aidha Mkurugenzi huyo aliongeza kwa kusema kuwa kwenye utafiti wao walibaini ushiriki wa wazazi kufuatilia maendeleo ya watoto wao ni mdogo jambo ambalo linapelekea watoto wengi kutofuatilia masomo yao kwa ufasaha lakini pia wengi wao kutohudhuria shule ipasavyo.
“Tumebaini Asilimia 50 ya wazazi hawafuatilii maendeleo ya watoto wao mashuleni hii inarudisha nyuma juhudi za serikali jambo ambalo watoto wengi huishia njiani masomo yao huku elimu ikiwa ni bure”,aliongeza.
Kwa Upande wake Meneja Uwezo Zaida Mgalla alisema kuwa utafiti huo waliufanya kwa wilaya 56 lakini waliona kuwa ufaulu umeongezeka kwa watoto wa darasa la tatu hasa kwenye somo la Kiswahili toka asilimia 29 kwa mwaka 2011 hadi kufikia 62 kwa mwaka 2017 ambapo kwa darasa la saba wengi wanamaliza wakiwa hawajui kusoma Kiswahili na kingereza.
“Utafiti huu tumeweza kufanya pia kwa vijiji 1680 na tuliweza kuhusisha wadau mbalimbali katika kufanya utafiti huo lakini tulibaini kuwa bado tuna idadi ya asilimia 64 ya watoto wanaomaliza darasa la saba bila kujua kusoma kwa ufasaha kingereza”,alisema Zaida.
Bi Mgalla alisema kuwa Utafiti huo walifanya kwa kutumia mtaala wa Serikali wa Darasa la pili hivyo ulitoa urahisi kwa watoto hao kuelewa maswali walioweza kuulizwa na wao kufanyia tathimini.
“Tulishirikiana Baraza la mtihani la Taifa kuweza kutumia mtaala wao ili kupata takwimu zilizo bora na zenye uwakika”,aliongeza.
Hata hivyo Utafiti huo ulifanyika kwa makundi Matatu ambapo ni watoto wenye Umri wa Miaka 9 hadi 13 waliopo shuleni na nje ya shule,Watoto wanaosoma shule walio darasa la tatu hadi saba na watoto ambao hawasomi shule kabisa wenye umri wa Miaka 9 hadi 13.