Na ASP. Lucas Mboje, Dar es Salaam
JUMLA ya Wafungwa 5,533 katika
magereza mbalimbali nchini walionufaika na msamaha wa Rais wakati wa
maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wameachiliwa huru magerezani.
Akizungumza na wanahabari leo
jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Phaustine
Kasike amesema kuwa utekelezaji wa zoezi la kuwaachiliwa huru wafungwa
wote walionufaika na msamaha wa Rais umekamilika nchi nzima.
“Ni matarajio yangu kuwa wafungwa
walioachiliwa wamejutia makosa yao na wataacha kutenda uhalifu hivyo
kujihusisha na shughuli halali kwa maendeleo yao, familia zao, jamii na
taifa kwa ujumla”, amesisitiza Jenerali Kasike.
Aidha, Kamishna Jenerali Kasike
ameelezea manufaa mbalimbali ya msamaha huo; mosi kupungua kwa
msongamano magerezani, pili, wanufaika wa msamaha kujumuika na familia
zao, tatu, kichocheo cha urekebishaji magerezani kwani msamaha huo
utasaidia kuimarika kwa nidhamu na kurejesha matumaini kwa wanaobakia
magerezani pamoja na wanufaika wa wamsamaha huo kupata fursa ya
kujishughulisha na shughuli za maendeleo uraiani.
“Zipo changamoto zilizojitokeza
katika utekelezaji wa zoezi hili ambapo baadhi ya wafungwa walionesha
kuwa hawako tayari kuungana na jamii zao pamoja na waliosamehewa kurejea
kutenda makosa mara baada ya kuachiwa huru. Hata hivyo nitoe wito kwa
jamii nchini kuwapokea wafungwa hao na kuacha kuwanyanyapaa”, amesema
Jenerali Kasike.
Wakati huo huo, Kamishna Jenerali
Kasike amemshukru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Dkt. John Pombe Magufuli kwa
kutoa msamaha huo ambao ni wa kihistoria hapa nchini. Pia amewapongeza
wanahabari wote nchini kwa namna walivyoshiriki kutoa habari za zoezi la
msamaha huo katika ngazi ya Mkoa na wilaya.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Ibara ya 45(1) (d) imempa mamlaka Rais kutoa
msamaha kwa wafungwa waliopo magerezani. Kwa kutumia Ibara hiyo Rais
Dkt. John Pombe Magufuli alitoa msamaha kwa wafungwa wakati wa
maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru ambapo kilele chake kilifanyika Mkoani
Mwanza Desemba 9, 2019.