Kiongozi
wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema hawajafanya mazungumzo
yoyote na waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye ambaye leo mchana
Jumatano Desemba 4, 2019 ametangaza kuwa si mwanachama wa Chadema.
Zitto
ametoa maelezo hayo saa chache baada ya Sumaye kumaliza kuzungumza na
waandishi wa habari na kueleza sababu za kujiondoa Chadema, moja ikiwa
ni hali ya sintofahamu iliyoibuka katika uchaguzi wa uenyekiti Kanda ya
Pwani ambao alipigiwa kura 48 za hapana kati ya 76.
Katika ukurasa wa mtandao wake wa kijamii wa Twitter, Zitto amesema; "Nipo
Mahakamani tangu asubuhi mpaka sasa nikiendelea na kesi ya uchochezi
dhidi yangu. Ninasikia tumetajwa tajwa kuhusu Mzee Sumaye. Itoshe kusema
kuwa Chama cha @ACTwazalendo hakina mazungumzo yeyote na Waziri Mkuu
huyo Mstaafu. Nashauri apewe nafasi ya kupumzika kama alivyoomba
Sisi
kama chama tumehuzunishwa na uamuzi wa Mzee Sumaye kupumzika Siasa.
Ilikuwa ni tunu katika upinzani kuwa na Waziri Mkuu Mstaafu katika ngazi
zake za Uongozi. Bila shaka tutachota maarifa na uzoefu wake kama
mwenyewe alivyoruhusu. Chama chetu kinaheshimu na kuthamini Wastaafu
Kwa
upande wangu nawatakia kila la kheri wenzetu wa CHADEMA katika Uchaguzi
wao unaoendelea. Dhamira yetu ya kuunganisha nguvu ya Vyama vya
upinzani ili kukabiliana na CCM haina mashaka. Mara baada ya Uchaguzi wa
wenzetu tutaendelea na mazungumzo ya ushirikiano na Uongozi mpya"