Kiti pekee kinachotumiwa na wakazi wa mtaa wa Majengo Kahama Mjini kwenye matukio ya misiba
Na Adela Madyane-Malunde 1 blog Kahama
Mgogoro baina ya Wananchi wa Mtaa wa Majengo na viongozi wa mtaa huo
umeibuka baada ya Nzengo hiyo kupatwa na msiba hapo jana na kukosa viti
vya kukalia, huku nzengo nzima ikimiliki kiti kimoja pekee.
Mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu sasa, umekuwa ukitokea mara tu
panapokuwa na msiba katika nzengo hiyo kutokana na uwepo wa kiti kimoja
ambacho hakikidhi mahitaji ya umati unaokuwa umehudhuria msibani.
Wananchi waliohudhuria msiba huo walisema mgogoro huo umesababishwa na
viongozi wa mtaa kushindwa kuhamasisha wananchi kuchangia ununuzi wa
viti jambo ambalo linapelekea kila unapotokea msiba katika eneo lao
mgogoro kuibuka juu la suala la kukosekana kwa viti kwa nzengo hiyo.
“Hili tatizo la ukosefu wa viti ni la muda mrefu sasa na linakera.
Tumemhoji mwenyekiti wa mtaa mara kadhaa na binafsi nimeona tatizo lipo
kwa viongozi wetu wa mtaa kwani wananzengo hawawezi kushindwa kuchangia
ununuzi wa viti,” alisema James Magini mkazi wa mtaa wa Majengo kati.
Naye Joramu Jumanne alisema ili kumaliza mgogoro huo viongozi wa Mtaa
kwa kushirikiana na viongozi wa Nzengo wanapaswa kutoa elimu kwa
wananchi juu ya ununuzi wa viti pamoja na vitu vingine kama maturubai,
na sio kuwalazimisha kutoa michango ya kununua viti pindi msiba
unapotokea kwani kwa kufanya hivyo shida inaweza kutokea.
“Changamoto zipo nyingi katika mtaa wa Majengo Kati zinazohitaji
vikao vya dharula ili viongozi na wananchi wakae meza moja kulipatia
ufumbuzi kwani ni muda mrefu Nzengo ina kiti kimoja atakayekiwahi ndiyo
huyo na hapa tuna watu wa kada mbalimbali katika nyadhifa mfano akija
mkuu wa Wilaya msibani mwananchi aliyekalia hicho kiti atalazimika
kukiachia bila kujali umri,” alisema Joramu.
Naye Balozi wa Nzengo ya Majengo Kati Donald Masele akizungumza na
waandishi wa Habari waliofika katika tukio hilo alikiri na kusema kuwa
uzembe unasababishwa na wao viongozi kushindwa kuweka mkazo kwa wananchi
juu ya uchangiaji wa viti jambo ambalo linazusha mgogoro.
“Viongozi tukiwa na mkazo viti vitapatikana kwenye nzengo yetu kwani
wananchi wapo tayari kuchangia lakini kumekuwa na uzembe katika kufanya
ufuatiliaji, na uzembe huu umesababishwa na wanakamati waliokabidhiwa
kusimamia jukumu hilo", alisema Masele Balozi wa Majengo Kati.
Masele aliongeza kuwa wakazi wa Majengo Kati wana pesa na wanamiliki
miradi mikubwa ya maendeleo hivyo hawawezi kushindwa kuchangia kiti
kimoja kwa kaya moja kwa thamani ya elfu 15,000/=.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Mtaa wa Majengo John Lwaga Kitambi alisema
Mtaa wake una nzengo zaidi ya tano alianza kuhamasisha uchangiaji wa
viti Majengo Kati na Majengo Mashariki na kubainisha kuwa Nzengo hizo
mbili mwitikio ni mbovu.
Alisema kuwa hatua itakayochuliwa kwa wananchi watakaokaidi kuanzia sasa
juu ya michango itokanayo na misiba ni kutunga sheria ndogo ndogo
itakayodhibiti hali hiyo ili wakienda tofauti hatua kali itachukuliwa
dhidi yake.