Aliyekuwa mstahiki meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Alex Kimbe akiwaaga watumishi
Wanahabari wakipiga picha meya Kimbe wakati kuingia kwenye gari yake binafsi
Kimbe akihojiwa na wanahabari
Watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa wakimsikiliza Kimbe
......................
ALIYEKUWA mstahiki meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kupitia chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) Alex Kimbe amekabidhi ofisi kwa mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Himid Njovu ikiwa ni pamoja na kufanya kikao cha mwisho na watumishi wote wa Halmashauri hiyo akiwaleza kuwa hana kinyongo ataendelea kutoa ushirikiano kwa maendeleo ya wananchi .
Akizungumza wakati wa kikao chake na watumishi hao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri hiyo Kimbe alisema kuwa baadhi ya maeneo ambayo walifanya mchakato kama huo wa kumwondoa mstahiki meya kama Dar es Salaam hadi leo vikao vya baraza la madiwani na vikao vya kamati mbali mbali havifanyiki kutokana na meya aliyeondolewa kugoma kukabidhi ofisi ila yeye ameona ni hekimu kuwa kuepusha mivutano ya kisiasa yenye lengo la kukwamisha maendeleo na kuamua kutumia busara yake kukabidhi ofisi kama alivyotakiwa kufanya hivyo .
'' Ikitokea vikao vya baraza la madiwani havifanyiki katika Halmashauri husika ni wazi maendeleo hayajakuwepo maana pasipo vikao vya madiwani hakuna kinachoendelea kwenye Halmashauri kwa hiyo nimefikiria kwa kina mahitaji ya wananchi wetu wa Manispaa ya Iringa na sasa barabara nyingi zimeharibika nawananchi wanahitaji kutatuliwa kero hizo za ubovu wa miundo mbinu na nyingine ambazo zote zinahitaji vikao vya madiwani vifanyike kwa hilo nimeona ni vema busara itumike ili maendeleo yafanyike na kutolewa kwwangu kusiwe mateso kwa wananchi wasio na hatia nimeamua kuja kukabidhi ofisi mambo yaendelee '' alisema Kimbe
Alisema kuwa ili shughuli mbali mbali za kimaendeleo ziweze kufanyika katika halmashauri hiyo ya Manispaa ya Iringa ni lazima madiwani wakae na maamuzi yafanyike ya kutenga bajeti ya shughuli za kimaendeleo na kuendelea na migogoro ya kugoma kutoka madarakani si tu unawakomesha madiwani wa chama cha mapinduzi (CCM) ambao walihusika kumtoa katika nafasi yake ila wanaoteseka ni wananchi wa Manispaa ya Iringa.
Kimbe alisema kuwa kwa lile tukio lililofanyika juzi machi 28 la kumtoa madarakani yeye kwa upande wake ameridhika nao na ameona si sahihi kung'ang'ania nafasi hiyo ambapo kimsingi ni nafasi ambayo alipewa na madiwani wenzake kuwasimamia ili kuongoza Halmashauri hiyo na sio nafasi ambayo wananchi walimchagua maana nafasi aliyoomba kwa wananchi ni nafasi ya udiwani wa kata ya Isakalilo ambao ataendelea nao hadi hapo muda wake utakapokoma miezi michache ijayo .
'' Kwa kuwa nimeridhika na mchakato wa kunitoa uliofanyika ambao nilipigiwa kura 14 za ndio kati ya kura 26 za wajumbe wote pamoja na kuwa kura za kunitoa zilipaswa kuwa kuanzia 17 ila sina kinyongo chochote na kutolewa kwangu kwa sababu wakubwa walitaka nitoke ili kujifurahisha na nafsi zao sitaki kuwakwaza nimetoka na leo nimeona nije kuwatia moyo watumishi wenzangu kwa ushirikiano mzuri mlionesha kipindi nikiwa meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa na nawaombeni mzidi kuwajibika kwa maslahi mapana ya wananchi wa Manispaa ya Iringa '' alisema Kimbe
Kuwa kwa upande wake ushauri ambao alikuwa akiutoa kwa Halmashauri ataendelea kuutoa na ataendelea kuonekana katika viwanja vya manispaa ya Iringa kama diwani wa kata ya Isakalilo na pale mkurugenzi wa Halmashauri hiyo na watumishi wengine watakapohitaji msaada wake wa kimawazo kwa ajili ya maendeleo ya wana Iringa atautoa na watumishi wasiogope kumuomba ushauri pale inapohitajika kufanya hivyo .
Aidha alisema kuwa kwa upande wake alikuwa na ndogo kubwa za kimaendeleo katika mji wa Iringa na miongoni mwa mikakati yake kupitia baraza la madiwani walikuwa wakitarajia kuwa na vitengo uchumi vingi kama ujenzi wa utawala ,jengo la biashara Tembo Bar na kwa kuwa sheria inamtaka yeye kama diwani kutoa ushauri wake kwenye baraza la madiwani ataendelea kufanya hivyo kwa faida ya wananchi wa Iringa .
Alisema jambo kubwa ambalo lilimsukuma kuagana na watumishi hao leo ni kutokana na ushirikiano mkubwa ambao alionesha wakati wote wa utawala wake kama mstahiki meya wa Halmashauri hiyo toka alipochaguliwa miaka mitano iliyopita kuongoza nafasi hiyo .
'' Nawaomba sana watumishi wote wa Manispaa ya Iringa msijisikie vibaya kuondolewa kwangu madarakani naomba mfanye kazi ya kuwatumikia wananchi kwa moyo wa kujituma zaidi kwani kuondoka kwangu kusiwe mwanzo wa watumishi kuvunjika moyo wa kufanya kazi ''
Kimbe alisema anachojivunia kwa utawala wake kama Mstahiki meya wa Manispaa ya Iringa kwa miaka yote minne halmashauri hiyo imekuwa ikipata hati safi na hata siku moja haikupata kufanya vibaya katika ukusanyaji wa mapato yake wala katika suala la usafi wa mji na anatamani wanaobaki kwa kipindi hiki kifupi kulinda heshima hiyo aliyoiacha.
Alisema kuwa akiwa Meya Halmashauri hiyo imepata kujenga shule nyingi za sekondari pia ujenzi wa Hospitali ya wilaya ya Frelimo ,vituo vya afya na miradi mingine mingi ya kimaendeleo ambayo imefanyika kwenye Halmashauri hiyo kama mradi mkubwa wa stendi ya mabasi Igumbilo ,soko la Kisasa la Mlandege pia matokeo ya mitihani ya darasa la saba kitaifa Manispaa ya Iringa imeendelea kufanya vizuri sana .
'' Natambua mazuri mengi yamefanyika ila kuondolewa kwangu hakuna baya nilillolifanya ila wakubwa hawakutaka Manispaa ya Iringa kuwa na meya wa Chadema kwa sababu ambazo wanazijua wao ila hakuna sababu nyingine ambazo zilifanya nitoke madarakani ila nachojivunia dunia yote inajua haya na kuondoka kwangu hivyo heshima yangu imeongezwa thamani na watalawa waliotaka nitoke madarakani ila wananchi wanatambua mimi bado ni meya wa mioyo yao leo nimekabidhi ofisi na gari naingia kwenye gari langu kuendelea na majukumu yangu ya udiwani na nitagombea tena udiwani Isakalilo katika uchaguzi mkuu ujao ''
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Himid Njovu alimpongeza Kimbe kwa maneno yake mazuri ya busara na kuwa anamkaribisha kuendelea kutoa ushirikiano kwa nafasi yake ya udiwani katika kuongoza Halmashauri hiyo