Miliki wa mtandao wa Jamii Forum Maxence Melo
...........................................................
Kesi namba 456 ya mwaka 2016 inayomkabili Ndg. Maxence Melo na mwenzake Micke William itasomwa leo Aprili 02, 2020 mbele ya Hakimu Thomas Simba kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Hukumu hii awali ilipangwa kutolewa Novemba 26, 2019 lakini iliahirishwa mara nne (4) kwa kigezo kwamba Hakimu alikuwa hajamaliza kuandika hukumu: Desemba 06, 2019, Januari 22, 2020 na Februari 19, 2020.
Historia ya kesi hiyo ni kwamba, Kampuni ya Oilcom iliandikwa katika mtandao wa Jamii Forums ikidaiwa kukwepa kulipa kodi na kuchakachua mafuta kwenye bandari ya Dar es Salaam.
Baada ya taarifa hizo kuandikwa kwenye mtandao wa Jamii Forums, polisi waliandika barua kwenda kwa Jamii Forums kuomba taarifa za mtu aliyeandika kuhusu Oilcom. Polisi hawakufanikiwa kupata taarifa hizo ndipo walipoamua kumkamata na kumuhoji Ndg. Maxence Melo bila mafanikio kwa mara nyingine ndipo alipofunguliwa shitaka la kuzuia upelelezi kwa kutokutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi alipotakiwa kutoa taarifa za aliyeandika kuhusu Oilcom kwenye mtandao wa Jamii Forums kinyume na kifungu namba 22(1) cha Sheria ya Makosa ya Mtandaoni ya Mwaka 2015.
Ndg. Maxence Melo alikamatwa mnamo Desemba 13, 2016 na kupelekwa gereza la keko kwa siku 3 bila ya kupewa dhamana, alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Desemba 16, 2016 na kufunguliwa kesi tatu (3) tofauti zenye shitaka moja la kuzuia upelelezi kwa kutokutoa ushirikiano polisi juu ya taarifa za walioandika kwenye mtandao wa Jamii Forums.
Aidha, Februari mwaka 2017 upande wa Jamhuri ulimuongeza Ndg. Micke William kwenye kesi hizo kama mmiliki wa hisa wa kampuni ya Jamii Media.
Kesi hizo ni zifuatazo: Mosi, Kesi namba 456 ya mwaka 2016 ambapo Ndg. Maxence Melo alishtakiwa kama Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Jamii Media kwa kosa la kuzuia upelelezi kwa kutokutoa ushirikiano kwa polisi juu ya taarifa za aliyeandika kuhusu Oilcom kwenye mtandao wa Jamii Forums. Katika nyakati tofauti za usikilizwaji wa kesi hii namba 456 upande wa Jamhuri umewahi kukiri kwamba Ndg. Micke William aliingizwa kimakosa kwenye kesi hiyo.
Pili, Kesi namba 457 ya mwaka 2016 ambapo washitakiwa walituhumiwa kwa kosa la kuzuia upelelezi kwa kutokutoa ushirikiano kwa polisi juu ya taarifa za aliyeandika kuhusu kampuni za CUSNA Investment na Ocean Link kudaiwa kukwepa kulipa kodi kwenye Bandari ya Dar es Salaam na kunyanyasa wafanyakazi wa kitanzania.
Uamuzi wa shauri hilo (shauri namba 457) ulitolewa Juni 01, 2018 ambapo Hakimu Godfrey Mwambapa aliamua kwamba Washitakiwa hawana kesi ya kujibu na hivyo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliwaachia huru.
Katika kesi hiyo pia, Polisi walitaka JamiiForums iwapatie taarifa za mwanzisha mada KWAYU na mchangiaji mmoja AMRISHIPURI ili waweze kuwakamata na kuwahoji kutokana na ukiukwaji wa taratibu, JamiiForums haikutoa taarifa binafsi za wanachama wake kwa kuamini kuwa chanzo hiki cha taarifa kilikuwa na nia njema hivyo kutaka kwanza iwepo Hati ya Mahakama inayoridhia kukamatwa kwa mhusika na kuelezwa kosa lake.
Tatu, Kesi namba 458 ya mwaka 2016 ambapo washtakiwa wanatuhumiwa kwa kosa la kuzuia upelelezi kwa kutokutoa ushirikiano kwa polisi kuhusu Benki ya CRDB ambapo Polisi ilimtaka Mkurugenzi wa JamiiForums kutoa taarifa kuhusu Wanachama wawili wa Mtandao wa JamiiForums walioandika kuhusu Benki ya CRDB.
Taarifa zilizotakiwa ni za Wanachama walioanzisha mijadala iliyosomeka "Charles Kimei (CRDB) jiuzulu, kashfa ya kontena, tiketi TFF, wanafunzi na ujambazi CRDB" mjadala unaodaiwa kuanzishwa tarehe 18 Januari 2016 pamoja na "Wizi wa Benki ya CRDB - Part II" unaodaiwa kuanzishwa Machi 11, 2015.
Taarifa za Wanachama ambazo zilitakiwa kutolewa ni IP-Address, barua pepe, Majina Halisi ya Wanachama hao. Kesi hii bado inaendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Huruma Shaidi.
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umekuwa ukifuatilia kwa ukaribu mwenendo mzima wa uendeshwaji wa kesi zote hizo.
*Imetolewa na*
*Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)*
*Aprili 02, 2020*