Ombaomba Mbeya waonywa kutembea na kundi la watoto wanapoomba mitaani

Na Joachim Nyambo,Mbeya.
OMBAOMBA MAARUFU JIJINI MBEYA ANUSURIKA KICHAPO MARA BAADA YA ...
Ombaomba Mkoani Mbeya

SHIRIKISHO la Vyama vya watu wenye ulemavu mkoani Mbeya limekemea vikali tabia ya baadhi ya walemavu kutumia mwanya wa watoto kutokwenda shule kutokana na Ugongwa wa Homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona kuwatumikisha kwa kuongozana nao mitaani wanakofanya shughuli za ombaomba.

Tangu Serikali ifanye uamuzi wa kufunga shule kuanzia za Awali,Msingi,Sekondari na vyuo hapa mchini,na kuwataka wanafunzi kubaki majumbani mwao ikiwa ni njia mojawapo ya kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima,mkoani Mbeya kwa upande wa wazazi wanaofanya shughuli za ombaomba wanaonekana kuitumia vibaya fursa hiyo kwa kuzurula na watoto wao.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Ofisini kwake,Katibu wa Shirikisho la Vyama vya watu wenye ulemavu mkoani hapa,Jimmy Ambilikile alisema kinachofanywa na wazazi hao ni jambo linalohatarisha maisha ya watoto wao.

Ambilikile alisema kama Shirikisho wamefuatilia kwa karibu na kushuhudia mara kadha wazazi na walezi wanaofanya shughuli za ombaomba hasa kwenye maeneo ya biashara wakiongozana na watoto wao pasipo kujali tahadhali zinazotolewa na Serikali na wadau wengine wa Sekta ya Afya.

Alisema hatari zaidi inakuja pale ambapo ombaomba hao ambao wengi wao ni wale wasioona hawaishii kuongozana na mtoto mmoja kwaajili ya kumuongoza bali huongozana na watoto wa familia yake yote hasa walio wadogo jambo alilosema tayari wanakuwa wamesababisha mkusanyiko mwingine.

Ambilikile ambaye pia ndiye Makamu Mwenyekiti wa Chama cha walemavu(Chawata) nchini na pia Mwenyekiti wa Chama chama hicho mkoa wa Mbeya alisema ni vema wazazi na walezi wakafuata utaratibu uliopangwa na Serikali wa watoto kubaki majumbani na kama wanahitaji wasaidizi basi watembee na mtoto mmoja na si kundi la wanafamilia kama inavyofanyika sasa.

“Utakuta mlemavu mmoja ameongozana na watoto watatu wane mpaka watano..hao wanatembea..bado kuna mdogo aliyembeba mgongoni sasa wanapoingia eneo la biashara kama dukani kuomba wakakutana na watoa huduma na wateja tayari huo ni mkusanyiko wenye hatari katika kipindi hiki.Haya watoto wenyewe kutokana na umri mdogo karibia kila eneo wanalopita wanataka kushika vitu watafungua milango na kumbuka wakipewa msaada wa vitu wanavishika na kunawakati hawanawi mikono yao..Sasa unaweza kuona mnyororo wa maambukizi unavyoweza kutokea iwapo katika moja ya maeneo waliyopita kuna Virusi vya Corona.”alifafanua Ambilikile.

Katibu huyo aliwataka walemavu wanaofanya shughuli za ombaomba kutambua kuwa kipindi hiki cha Mapambano dhidi ya Corona ni hatari na kinahitaji umakini mkubwa kwa kufuata maelekezo yanayotolewa kila wakati.

Alisema kuachana na mazoea kutaiwezesha jamii kuwa salama na hatimaye kuivusha katika kipindi kigumu kinachoendelea alichosema kila mmoja anapaswa kwa nafasi yake kujiuliza anafanya nini kujikinga yeye,familia yake na jamii inayomzunguka.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post