Na Joachim Nyambo,Mbeya.
Kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi Kamanda wa Polisi Jiji la Mbeya Ulrich Matei akizungumza na waandishi wa habari |
JESHI la Polisi mkoani Mbeya limeonya mikusanyiko ya
aina yoyote siku ya Sikukuu ya Pasaka ikiwemo Disco toto na kuonya kuwa yeyoto
atakayeandaa burudani ya aina hiyo basi huyo atatumika kuwa fundisho kwa
wengine.
Kadhalika limesema katika kukabiliana na maambukizi
ya Covid 19 wazazi na walezi wote mkoani hapa wanapaswa kuchukua tahadhali kwa
kuwalinda watoto wadogo kwa kuhakikisha muda wote wako majumbani badala ya kuwaacha
nje.
Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya,Ulrich Matei alitoa
onyo hilo alipozungumza na waandishi wa habari ambapo alisema Jeshi hilo
halijatoa kibali chochote cha Disco toto wala mikusanyiko ya aina yoyote ya
burudani.
Kamanda Matei alisema kipindi hiki cha Sikukuu ni
muda ambao wazazi na walezi wanapaswa kuchukua tahadhari kwa kiasi kikubwa hasa
kwa watoto wadogo wasiowezaq kujifanyia maamuzi kwakuwa wanaweza kupelekwa
kwenye maeneo hatarishi na ndugu zao wa karibu wasiojali usalama wao.
Aliongeza kuwa tahadhali zaidi inapaswa kuchukuliwa
juu ya maambukizi ya ugonjwa huo hasa kwa kuzingatia kuwa mkoa wa Mbeya
umepakana na nchi jirani ya Malawi,mikoa iliyo jirani na nchi jirani kama mkoa
wa Songwe na Rukwa inayopakana na nchi za Zambia na Congo DR pamoaj na uwepo wa
barabara kuu inayopitisha wageni wengi.
“Nasisitiza kuwa hadi sasa hatujatoa kibali chochote
kwaajili ya Disco toto wala mikusanyiko mingine.Muhimu kwa wazazi na walezi
katika siku hiyo ni kuhakikisha watoto wao hasa wadogo wanakuwa ndani muda wote
chini ya uangalizi.Wasiwaache watoto wakazurula au kuwatumatuma.Maana kwa wtoto
wadogo unaweza kumtuma kufika huko akakutana na vitu vingine vikamshawishi na
kujikuta wametengeneza mkusanyiko wao.”
“Lakini pia tunawasihi wazazi na walezi hawa
kuchukua tahadhari kwa kutokwenda na watoto wadogo kwenye mikusanyiko au kwenye
maeneo ya starehe.Kipindi hiki ni vema kila mmoja akabakia kwake na watoto
wake.” Alisisitiza kamanda Matei.
Akizungumzia suala la usalama barabarani,kamanda
huyo aliwataka watumiaji wote wa barabara kulinda usalama wao na wa wengine
huku akisema ulinzi pia utaimarishwa katika maeneo ya miteremko mikali hususani
Mlimanyoka,Igawilo,Iwambi na Mwansekwa.
Kwa upande wa nyumba za ibada,Matei alisema pia
ulinzi utaimarishwa lakini akasisitiza kuwa ni muhimu waumini watakaoshiriki
ibada za sikukuu wakazingatia ushauri unaotolewa na Serikali sambamba na wizara
ya Afya ili kujilinda dhidi ya Corona.