Wazazi waaswa kutoficha watoto wenye midomo sungura

kijana mwenye mdomo sungura
Na Joachim Nyambo,Mbeya.

WAKAZI wa mikoa ya Nyanda za juu kusini wametakiwa kuitumia fursa ya utoaji bure Huduma ya Matibabu ya Mdomo Sungura inayofanyika katika Hospitali ya Rufaa kanda ya Mbeya(MZRH) kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la Kimarekani la Smiletrain.

Rai hiyo imetolewa na Mtaalamu wa Upasuaji wa Mdomo Sungura katika Hospitali ya Rufaa kanda ya Mbeya,Dkt Omary Matola alipozungumzia Mradi wa Utoaji wa huduma hiyo unaoendelea katika hospitali hiyo.

Dk Omary alisema bado wapo wazazi na walezi wanaoendelea kuamini kuwa katika familia au ukoo kuzaliwa kwa mtoto aliye na tatizo la mdomo Sungura ni nuksi na hivyo baadhi yao kuwafungia ndani watoto hao.

Alisema ni wakati kwa jamii kuachana na dhana hizo potofu na badala yake kuzitumia fursa za utoaji bure wa huduma za upasuaji katika hospitali mbalimbali nchini zinazotoa huduma hiyo ikiwemo MZRH.

Alizitaja Hospitali nyingine zinazotoa huduma hiyo bure kwa sasa hapa nchini kuwa ni KCMC ya mkoani Kilimanjaro,Bugando ya Mwanza,Siriani Arusha,Dodoma,Tumbi mkoani Pwani na CCBRT jijini Dar es salaam.

“Mdomo sungura ni tatizo la kuzaliwa kama matatizo mengine na linatibika.Tuachane na dhana kuwa ukizaa mtoto mwenye tatizo hili kuwa ni nuksi kwenye ukoo au familia.Ni jambo la kusikitisha mpaka leo hii pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali na wadau wengine bado kuna watu wanawafungia ndani watoto wenye matatizo haya.”Alisema Dkt Omary.

Aliyataja matatizo anayokumbana nayo mtoto mwenye mdomo sungura kuwa ni pamoja na kushindwa kunyonya hasa kwa wale walio na mdomo wazi wa ndani,kupata maambukizi ya sikio na kupelekea usikivu finyu,matatizo ya kinywa na meno,na kama atakosa matibabu ya mapema atakuwa na matatizo kwenye uzungumzaji na pia unyanyapaa.

Hata hivyo Dkt Omary alisisitiza mambo yanayopaswa kuzingatiwa kabla ya mtoto kupelekwa Hospitalini kwaajini ya upasuaji wa mdomo sungura kuwa ni pamoja na mtoto awe ametimiza umri wa miezi mitatu,awe na uzito usiopungua kilogramu tano na uwingi wa damu usiwe chini ya 10.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post