Katibu Mkuu wa Chama
cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA), Suleiman Msuya
kushoto akimkabidhi Bw John Bukuku Mkurugenzi wa Fullshangweblog na
Fullshangwe tv Barakoa ambazo zimetolewa kwa waandishi wa habari wa
vyombo mbalimbali kutoka kiwanda Cha maziwa Cha ASAS Cha mkoani Iringa
leo jiini Far es salaam.
………………………………………………………..
NA MWANDISHI WETU
KAMPUNI ya ASAS
imetoa msaada wa Barakoa (Masks) 1,000 kwa waandishi wa habari wa vyombo
mbalimbali vya habari vya jijini Dar es Salaam ili waweze kujikinga na
maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID-19.
Msaada huo umetolewa
na kampuni hiyo kwa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo Habari Tanzania
(JOWUTA), ili kuwapatia wanachama wake na waandishi kwa ujumla.
Akizungumzia msaada
huo Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Kampuni ya ASAS, Ahmed Salim alisema
wameamua kusaidia kundi hilo kutokana na mchango wake kwa jamii katika
kipindi hiki cha corona.
Mkurugenzi huyo
alisema waandishi wa habari kazi zao zinahitaji kukutana na watu
mbalimbali hivyo wanapaswa kuwa na vifaa vya kujikinga na maambukizi
hivyo kampuni hiyo inaamini imetoa msaada sehemu sahihi.
“Nyie ni watu muhimu
katika kuhabarisha jamii kuhusu maambukizi ya corona hivyo ni imani yetu
kuwa Barakoa hizi 1,000 zitasaidia kwa muda na tutaendelea kushirikiana
na JOWUTA kusaidia hali ikiruhusu,” alisema.
Salim alisema iwapo
waandishi watapata maambukizi jamii itakosa taarifa sahihi za COVID-19,
hivyo kuwataka wadau wengine kulisaidia kundi hilo muhimu kwa maendeleo
ya nchi na wananchi.
Mkurugenzi huyo
aliwaomba waandishi kuzingatia misingi, kanuni na sharia zinazosimamia
taaluma yao kwa kuandika habari za kweli ili kutopotosha wananchi.
“Tumekuwa tukitoa
misaada kama hii kwa makundi mbalimbali, hivyo basi sisi tunaamini nyie
ni watu sahihi na mtazitumia kwa maslahi mapana ya kazi zenu kwa
kuzingatia maadili,” alisema.
Alisema wametoa
Barakoa, vitakasa mikono, mashine ya kupulizia mwili mzima, ndoo na
vingine lengo likiwa ni kusaidia jamii ambayo kwa namna moja au nyingine
inatumia malighafi za ASAS.
Akizungumzia msaada
huo Katibu Mkuu wa JOWUTA, Suleiman Msuya alipongeza Kampuni ASAS
kuwakumbuka waandishi wa habari wa Dar es Salaam ambao walikuwa
wanapitia changamoto ya uhaba wa vifaa hivyo.
Msuya alisema
waandishi wa habari walikuwa wanapata wakati mgumu wa kutafuta habari
kutokana na mambukizi ya corona kusambaa jijini Dar es Salaam lakini
kupitia msaada huo wa ASAS watakuwa wamepata suluhu kwa muda.
“Tunaishukuru Kampuni
ya ASAS kwa msaada huu wa Barakoa 1,000 zitatusaidia sana katika
kipindi hiki kigumu naamini sasa tutafanya kazi kwa uhuru na hata
tukiandika habari na makala za kusisitiza uvaaji barakoa tunaonekana kwa
mfano,” alisema Msuya.
Katibu huyo aliwataka
waandishi wa habari na vyombo vya habari nchini kuzingatia maandili ya
uandishi hasa katika kipindi hiki ambacho dunia inapitia wakati mgumu.
Msuya alitoa rai kwa waandishi wa habari kuepuka kutumika katika kipindi hiki kwani madhara yake yanaweza kuwa makubwa.