BAJETI 2020/2021 KUSOMWA LEO

Macho  na masikio yanatarajiwa kuelekezwa bungeni jijini Dodoma leo wakati serikali itakapowasilisha makadirio ya bajeti yake kwa mwaka ujao wa fedha.

Mpango wa Maendeleo ya Taifa na ukomo wa bajeti ya mwaka 2020/21, unaonyesha bajeti hiyo inatarajiwa kuwa ya Sh. trilioni 34.88, huku Sh. trilioni 21.98 zikitengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, ikiwamo gharama za uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Bajeti hiyo ya mwisho kwa awamu ya kwanza ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli, imeongezeka kutoka Sh. trilioni 33.1 zilizotengwa kwa mwaka huu wa fedha (2019/20), sababu kuu ikitajwa kuwa gharama za uchaguzi mkuu.

Mbali na uchaguzi mkuu, bajeti hiyo pia imezingatia mahitaji halisi ya ugharamiaji miradi mikubwa ya kimkakati, ulipaji mishahara, deni la serikali na vipaumbele vingine vya taifa.

Kwa mujibu wa mpango huo uliowasilishwa bungeni Machi 11, mwaka huu, kiasi cha Sh. trilioni 34.88 kinachotarajiwa kukusanywa, kinajumuisha mapato ya ndani ya Sh. trilioni 24.07 (asilimia 69 ya bajeti yote), mikopo ya ndani Sh. trilioni 4.9, mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara Sh. trilioni 3.04 na misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo Sh. trilioni 2.87 (asilimia 8.2 ya bajeti yote).

Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, kati ya fedha hizo, Sh. trilioni 21.98 zitakuwa za matumizi ya kawaida na Sh. trilioni 12.9 za matumizi ya maendeleo (asilimia 37 ya bajeti yote).

Bajeti ya maendeleo inajumuisha Sh. trilioni 10.16 ambazo ni fedha za ndani (asilimia 78.8 ya bajeti ya maendeleo) na Sh. trilioni 2.74 fedha za nje.

Pia Sh. bilioni 400 zitatumika kulipa madeni yaliyohakikiwa, ujenzi wa reli ya kati ya kisasa (SGR) Sh. trilioni 2.1, mradi wa umeme wa Julius Nyerere Sh. trilioni 1.6 na mingine ni Sh. trilioni 6.06.

Katika bajeti hiyo, kunatarajiwa kuwa na ongezeko na punguzo la tozo, ada na ushuru katika bidhaa mbalimbali zinazozalishwa ndani na nje ya nchi kama ilivyokuwa katika bajeti zilizopita.

Bidhaa zinazotarajiwa kuguswa ni pamoja na vinywaji baridi (soda, maji na juisi), sigara, mvinyo, pombe na pombe kali.

Maeneo mengine muhimu yanayotarajiwa kuguswa ni unafuu wa kodi kwenye sekta ya viwanda, kilimo, mifugo, madini na huduma muhimu za kijamii kwa lengo la kudhibiti mfumuko wa bei na kulinda viwanda vya ndani.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha, aliweka wazi kuwa bajeti ijayo ya serikali itakuwa na punguzo la tozo, ada, kodi na ushuru kwenye sekta anazozisimamia (mifugo na uvuvi).

Serikali pia inatarajiwa kuondoa migongano ya sheria, kanuni na taratibu zinazotumiwa na mamlaka mbalimbali katika utozaji kodi na gharama kubwa za kuanzisha na kuendesha biashara kutokana na wingi wa kodi, ada na tozo zinazoambatana na taratibu zenye urasimu.

Vilevile, Sera ya Bajeti inabainisha kuwa kwa mwaka ujao wa fedha, serikali inatarajiwa kuwa na bajeti yenye mikakati ya kuondoa mianya na mazingira ya rushwa na mwingiliano wa majukumu na wingi wa mamlaka za udhibiti katika kuidhinisha na kutoa hati, vibali na vyeti kwenye shughuli za uwekezaji na biashara.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post