Rais Magufuli amemtumbua hadharani Katibu Tawala wa Wilaya ya Kisarawe (DAS ), Mtela Mwampamba na kumteua Mwanana Msumi kushika nafasi hiyo hapo hapo.
Mwambapa ametumbuliwa leo tarehe 28 Juni 2020, wakati Rais Magufuli akizindua mradi wa maji wilayani humo katika Mkoa wa Pwani.
“Lakini pia hapa kuna tatizo moja, la mteule wangu mmoja DAS, ninaambiwa ana mambo ambayo hayaendani na maadili ya kazi yake, zipo tuhuma kwamba anachukua hata wake za watu. nilikwishamuonya siku za nyuma, nafikiri hakuweza kuonyeka.
“Na kwa sababu jukumu langu ni pamoja na kusimamia maadili na nidhamu za watendaji, ninakuagiza mheshimiwa Jafo (Suleiman Jafo – Waziri wa TAMISEMI) uongee na mheshimiwa Mkuchika (George Mkuchika, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora) kwamba huyu kazi ya U-DAS nimeitengua leo,” amesema Rais Magufuli.
Pia Rais Magufuli ameagiza Mwampamba atafutiwe kazi ya chini inayoendana na uwezo wake, lakini pia kazi hiyo asifanye ndani ya Wilaya ya Kisarawe. wa Mkoa.
Mara baada ya kauli hiyo Rais Magufuli akamteua muda huo huo, aliyekuwa Afisa Tawala wa Wilaya ya Kisarawe Mwanana Msumi kuchukua nafasi hiyo.