Na John Walter-Babati
Watu watatu wamekufa katika ajali ya barabarani iliyotokea katika kata ya Mamire wilayani Babati mkoani Manyara.
Akitoa taarifa leo June 16.2020, Kamanda wa polisi mkoa wa Manyara Paul Kasabago amesema, ajali hiyo iliyotokea june 13 mwaka huu, imehusisha gari lenye namba za usajili SU.417 aina ya Toyota Land Cruiser mali ya shirika hifadhi za Taifa (TANAPA), iliyokuwa katika doria maalum katika maeneo hayo yanayopakana na hifadhi ya Taifa ya Tarangire majira ya saa 2:45 usiku.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Manyara Paul Kasabago akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, amesema gari hilo lililokuwa linaendeshwa na dereva ambaye bado majina yake hayajafahamika, iligonga pikipiki yenye namba za usajili MC 313 BKU aina ya Boxer iliyokuwa ikiendeshwa na Said Ally (35) mkazi wa Mamire akiwa amewapakia abiria wawili (mshkaki) kinyume na sheria za usalama barabarani.
Kasabago amesema kuwa dereva wa pikipiki hiyo na abiria wote wawili aliokuwa amewabeba walipoteza maisha papo hapo.
Aidha Kamanda Kasabago ametaja majina ya waliopoteza maisha ni Said Ally (35), Elimina Herman (22) na Renatha Salutali (17) wote wakazi wa kijiji cha Mamire.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Paul Kasabago, mtuhumiwa alitoroka mara baada ya kusababisha ajali hiyo na kwamba jeshi hilo kwa kushirikiana na wananchi wanaendelea kumtafuta ili kujibu tuhuma zinazomkabili.
Kamanda ameeleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari hilo kushindwa kuchukua tahadhari za usalama bara barani.
Miili ya marehemu imefanyiwa uchunguzi wa kidaktari na kukabidhiwa ndugu kwa mazishi.