Na Seif Mangwangi, Arusha
MAHAKAMA ya sheria ya Afrika mashariki imetupilia mbali ombi la serikali ya Tanzania kupinga hukumu iliyotolewa na mahakama hiyo, ikitaka baadhi ya vifungu ya sheria ya huduma ya habari ya mwaka 2016 virekebishwe.
Pamoja na mambo mengine sheria hiyo inatajwa kukiuka mkataba wa Afrika mashariki pamoja na kuminya uhuru wa kupata habari.
Akitoa hukumu hiyo iliyosomwa kwa njia ya video kutokana na hofu ya maambukizi ya Corona, Jaji Kiongozi katika kesi hiyo Godfrey Kiryabwire alisema nia ya Serikali ya Tanzania kukata rufaa inatupiliwa mbali kutokana na kutokidhi matakwa ya kisheria.
"Mahakama imeamua kuwa nia ya rufaa ya serikali ya Tanzania inatupiliwa mbali kwa sababu ya kutokidhi baadhi ya matakwa ya kisheria.” Jaji Godfrey Kiryabwire amesema hayo kwenye hukumu aliyoitoa mahakamani.
Kesi hiyo iliwasilishwa katika mahakama hiyo na baraza la habari Tanzania MCT, mtandao wa watetezi wa haki za binadamu pamoja na kituo cha sheria na haki za binadamu, iliyopinga nia ya serikali ya Tanzana ya kukataa rufaa kupinga maamuzi ya mahakama yaliyowapa ushindi MCT na washirika wake mwaka jana 2019.
Kabla ya kufunguliwa kwa kesi hiyo, mwaka 2017, Baraza la habari Tanzania pamoja na watetezi wa haki za binaadam walipeleka maombi katika mahakama ya Afrika Mashariki kupinga vifungu kadhaa vya sheria ya huduma ya habari ya mwaka 2016 wakidai kuwa vinakinzana na vifungu vya mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki
Katika shauri hilo, mahakama ya Afrika Mashariki ilitoa ushindi kwa MCT na washirika wake dhidi ya Serikali ya Tanzania ndipo Serikali ya Tanzania ikapelekea ombi la kukata rufaa kupinga maamuzi hayo.
Kutokana na Mahakama hiyo kutupilia mbali nia ya Serikali ya Tanzania kukata rufaa,sasa watetezi wa haki za binaadam wanasema sheria hiyo inatakiwa kufanyiwa marekebisho.
Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania mara baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Baraza linajipanga kuwaelimisha wanahabari na wadau wa habari kuhusu vipengele 16 vinavyotakiwa kubadilishwa na wanaimani kuwa Serikali itatoa ushirikano wa kutosha kutekeleza maamuzi yaliyotolewa na mahakama hiyoya Afrika Mashariki.