Mahakama Yaipa Serikali Siku 7 Kesi Ya Tundu Lissu

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, inatarajia kuanza kusikiliza maombi ya wadhamini wa aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ambao wanataka mshtakiwa huyo akamatwe ili wajitoe udhamini.

Maombi hayo namba 2/2020 yalikuja jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba ambapo upande wa Jamhuri uliomba kuongezewa muda wa kuwasilisha majibu ya kiapo kinzani.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon aliiomba mahakama iwaongezee muda ili waweze kuwasilisha majibu ya kiapo kinzani kutokana na maombi yaliyowasilishwa na wadhamini hao.

Hakimu Simba alikubali maombi hayo na kuwapa upande wa Jamhuri muda ambapo wametakiwa ndani ya siku saba wawe wamewasilisha majibu hayo na maombi yatasikilizwa Julai 14.

“Kesi ya msingi namba 208 ya mwaka 2016 itatajwa Julai 14 mwaka huu ikisubiri maombi kusikilizwa na kutolewa uamuzi,” alisema Hakimu Simba.

Februari mwaka huu, wadhamini wa Lissu kwa nyakati tofauti waliieleza mahakama kuwa wamewasilisha maombi mahakamani hapo kuomba itoe hati ya kukamatwa Lissu ili waweze kujitoa udhamini kutokana na mtuhumiwa huyo kutohudhuria katika kesi yake.

Wakili Wankyo alikiri kupokea maombi yaliyoambatanishwa na hati ya kiapo na kuomba mahakama iwape muda wa kutosha waweze kuyachambua.

“Tumepokea hati ya kiapo cha maombi ya wadhamini, tunaomba mahakama itupe muda wa kutosha ili tuweze kuchambua maombi hayo kwa sababu yana vitu vingi,” alidai Wankyo.

Lissu na wenzake wanne katika kesi ya msingi, wanakabiliwa na mashtaka matano, ikiwamo kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Inadaiwa kati ya Januari 12 na 14, 2016 Dar es Salaam, washtakiwa Jabir Idrisa, Simon Mkina na Lissu waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho ‘Machafuko yaja Zanzibar’.

Katika shtaka la pili, wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Mshtakiwa Ismail Mehboob ambaye ni mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, anadaiwa kuwa Januari 13, 2016 katika jengo la kampuni hiyo lililopo Manispaa ya Ilala, alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa na taarifa za uchochezi.

Ilidaiwa mshtakiwa huyo pia alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post