SERIKALI KUWASHIKA MKONO WATAALAMU WA TIBA ASILI NCHINI

Na. Majid Abdulkarim, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametoa maelekezo kwa Wizara ya Afya kuwa kitengo cha dawa asili kiendelezwe kwa nguvu zote na bajeti iongezwe ili watu wanapotengeneza dawa zao wasidharaulike.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma wakati akizindua Jengo la Ofisi za TARURA zilizojengwa kwenye mji wa kiserikali – Mtumba.

Aidha Rais Magufuli amesema kuwa  Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inatakiwa  kuweka nguvu kwa kuongeza  bajeti katika Kitengo cha Tiba asili/tiba mbadala ili kutengeneza dawa za asili kwa ajili ya kuponya magonjwa mbalimbali nchini.

Rais Magufuli akizungumza amesema kuwa dawa za asili zinasaidia kutibu magonjwa mbalimbali  na kwamba zimesaidia kupambana na maambukizi ya virusi vya Corona nchini.

“Watanzania tubadilike na tupende dawa za asili zinazotengenezwa nchini kwani tumekuwa tukipumbazwa tusiamini dawa hizo, hivyo tuziamini na kuzitumia kwa kuwa zinaponya”, ametoa wito Rais Magufuli.

Pia Rais Magufuli amebainisha kuwa  Tanzania imepata fedha za msamaha kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) kwa kuidhinisha Dola 14.3 milioni za msamaha wa madeni kwa Nchi ya Tanzania kwa kuwa Nchi yetu imeweza kupambana vizuri na ugonjwa wa corona.

“Nitamuandikia barua Mkurugenzi Mkuu wa IMF kwa niaba ya Watanzania kumshukuru,fedha za IMF tutazitumia kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa wa corona, na maendeleo mengine yatakayosaidia corona isirudi tena katika nchi yetu” ameweka wazi Rais Magufuli.

Katika hatua nyingine Rais Magufuli amewataka Maofisa Tarafa Nchini kuzitunza pikipiki 448 alizowakabidhi mapema leo hii kwa lengo la kuwahudumia wananchi.

Niwatake Maofisa Tarafa wote Nchini, mkazitunze pikipiki hizi,na sio kupakizana Mishikaki au kuzitumia kwa matumizi yasiyofaa, hata kama wewe Ofisa ni mwanamke usiiache hiyo pikipiki tafuta msaidizi wako akuendeshe na uweze kufanya kazi za umma kwa ufanisi”, amesisitiza Rais Magufuli.

Rais Magufuli ameelekeza Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuweka utaratibu wa kuaandikisha maofisa tarafa hao kipindi watakapokabidhiwa pikipiki hizo ili kuweza kuwa na ushahidi pale kutakapo tokea uharibifu wowote katika pikipiki hizo au kuipoteza basi muhusika anatakiwa kuwajibika juu ya uharibifu huo ikiwa ni pamoja na kuilipa endapo itakua ameipoteza.

Katika hatua nyingine Rais Magufuli amewapongeza watendaji wa TARURA kwa kukamilisha ujenzi wa jengo lao na kuwataka kutumia fedha zinazoletwa na Serikali kutekeleza miradi ya barabara za mjini na vijiji kwa ufanisi.

Awali Rais Magufuli aliwataka  wananchi wote waliohudhuria hafla hiyo kutoa heshima ya kuwaombea aliyekuwa Rais wa Burundi Mhe. Piere Nkurunziza aliyetutoka siku chache zilizopita pamoja na Watu Nane waliofariki Dunia baada ya hiace waliyokua wamepanda kugongwa na Lori huko Mkoani Mwanza.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo amesema takribani bilioni 89.1 ni fedha iliyotengwa kwa ajiri ya kukamilisha mtandao wa barabara za lami kilomita 51.2 katika mji wa kiserikali.

“Mhe. Rais, nikuhakikishie kuwa barabara hizo ulizoziwekea jiwe la msingi leo zitapambwa na miti ya matunda pembeni na taa zaidi ya 700 za barabarani ili kuleta hadhi katika Jiji la Dodoma kuwa makoa makuu ya nchi yetu,” amesema Mhe. Jafo.

Awali akisoma taarifa ya ujenzi wa jengo hilo Mkurugenzi Mtendaji wa TARURA Mhandisi Victor Seif amesema jengo hilo lina sakafu(Flow) 3 na limejengwa kwa kutumia mfumo wa Force Account na umegharimu takribani shilingi Bil 1.9.

Awali kabla ya hafla hiyo Rais Magufuli ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Barabara za lami a mzunguko zenye urefu wa kilomita 51.2 katika mji wa Serikali Mtumba zinazojengwa na kusimiwa na TARURA.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post