Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha Mussa Matoroka |
Jumla ya wanachama 434 wa majimbo na viti maalum walichukua fomu za kugombea ubunge tangu zoezi hilo lilipoanza Julai 14, mwaka huu na hadi saa 10 jioni leo ni wanachama 432 waliojaza na kurudisha fomu hizo. Wanachama wawili, mmoja kutoka Arusha mjini na mwingine wa Monduli hawakurudisha fomu hizo.
Katibu wa CCM mkoa wa Arusha,Musa Matoroka, amewaambia waandishi wa habari ofisini kwake kuwa chama hicho kimeridhishwa na mwitikio wa wanachama wake katika kugombea nafasi za ubunge na udiwani na kwamba hiyo ni dalili ya kukomaa kwa demokrasia ndani ya chama hicho tawala.
"Tumeridhishwa na mchakato na tunawapongeza sana wana CCM kwa ukomavu wa kisiasa walioonyesha na sasa tunaingia katika hatua nyingine za kukamilisha mchakato wa kupata wagombea wetu katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, " amesema.
Matoroka alitaja idadi ya wagombea waliochukua fomu na kurudisha katika majimbo yao kuwa ni Arusha mjinj(91), Arumeru Magharibi (61),Arumeru Mashariki (33),Karatu (53), Ngorongoro (14), Longido (12) na Monduli (24).
Kwa upande wa Viti Maalum, Katibu huyo amesema upande wa Vijana wamechukua fomu wagombea 30 na wote wamerudisha,Wazazi wagombea tisa na UWT ambayo inajumuisha makundi maalum wanachama 114 wamechukua na kurudisha fomu za kugombea ubunge.
Kuhusu madiwani, Matoroka amesema takwimu za waliochukua zitajulikana baada kukusanya kutoka kata zote 158 za mkoa huo.
Amesema mikutano ya kura za maoni ya majimbo yote saba itafanyika Julai 20 hadi 21,mwaka huu.