Tanzania Pekee Yatajwa Kutokuwa na Corona Ulimwenguni

Na Seif Mangwangi

Ripoti iliyotolewa hivi karibuni na Kituo cha Bara la Ulaya cha Kuzuia na Kudhibiti magonjwa (ECDC) na baadaye ripoti hiyo kuchambuliwa na kusomwa na kituo kikubwa cha habari cha nchini Ujerumani cha Deutsche Welle (DW) imeitaja Tanzania kuwa nchi pekee duniani ambayo haijaripoti maambukizi yoyote ya mgonjwa wa Corona kwa wiki nne (4) zilizopita huku ikiwa salama na ugonjwa huo hatari duniani kwa sasa kwa takribani wiki 46.

Ripoti hiyo iliyotolewa na kituo hicho chenye makao makuu yake jijini Solna nchini Sweden, inaeleza kwamba wakati dunia nzima ikiwa kwenye giza totoro na isijue la kufanya kwa kuendelea kuripoti maambukizi ya Corona kila kukicha, Tanzania iko salama kabisa na balaa hilo na watu wakiendelea na shughuli zao za kila siku bila ya vizuizi wala masharti yoyote ya Corona.

Wakati Tanzania ikitajwa kutokuwa na virusi vya ugonjwa wa Corona, Nchi nyingi za Afrika zimeendelea kupokea msaada kutoka China kukabiliana na janga la Corona.

Hivi karibuni China imewasilisha msaada wa vifaa vya matibabu nchini Uganda na kukabidhi kwa waziri wa afya wa nchi hiyo Bibi Ruth Aceng.

Balozi wa China nchini Uganda Bw. Zheng Zhuqiang amesema vifaa hivyo ni pamoja na barakoa za upasuaji elfu kumi, barakoa za N95 elfu mbili, mavazi ya kujikinga ya kutumia mara moja elfu mbili, vipimia joto mia tano, miwani ya usalama elfu mbili, glavu za upasuaji elfu kumi, na kusema shehena ya pili ya msaada huo itawasilishwa hivi karibuni nchini Uganda.

Bibi. Aceng ameishukuru China kwa kuendelea kuiunga mkono Uganda haswa katika mapambano dhidi ya virusi vya Corona.

Wakati huohuo ubalozi wa China umetoa msaada wa dawa na vifaa vya kupambana na Corona kwa ajili ya watoto wa Ghana. Waziri wa jinsia, watoto, na ulinzi wa jamii wa Ghana Bibi Cynthia Morrison ameishukuru China kwa msaada huo.

Msaada kama huo pia umepokelewa nchini Senegal, ambako waziri wa afya wa Senegal Bw. Abdoulaye Diouf Sarr ameishukuru China kwa msaada huo na mshikamano inaoonyesha wakati wa mapambano dhidi ya janga la Corona.

Tanzania kupitia kwa Rais Dkt John Pombe Magufuli alitoa agizo la misaada mbalimbali kutoka nje ya nchi kufanyiwa uchunguzi kabla ya matumizi yake ili kuepuka kupata maambukizi mapya kama ambavyo imekuwa ikitokea katika nchi nyingi duniani.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post