WAJAWAZITO KUSAFIRISHWA KWA BODABODA NA POWERTILLER KWA WAKERA WAZEE MBARALI, WATAKA UJENZI WA ZAHANATI UKAMILISHWE

Wazee wakionesha bango kutaka zahanati.
Jiwe la msingi lililowekwa na kiongozi wa Mbio za mwenge wa Uhuru mwaka 2013,Rachel Kasanda kwenye jengo la zahanati ya Azimio Mswiswi.(Picha zote na Joachim Nyambo)

Mwenyekiti wa kijiji cha Azimio Mswiswi kilichopo katika kata ya Kongolo wilayani Mbarali,Aliagiza Ngwipa akitoa maelezo ya ujenzi wa Choo katika Mradi wa ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho wakati wajumbe wa Baraza la wazee la kata hiyo walipoambatana na wadau mbalimbali wakiwemo wataalamu wa afya ngazi ya wilaya na mkoa kutembelea mradi huo ambao awali ulikwama mwaka 2014 baada ya kuwekewa jiwe la Msingi na Mbio za Mwenge wa Uhuru na sasa wananchi wameamua kuuendeleza.(Picha na Joachim Nyambo)
 

Jengo la zahanati lililotelekezwa.

 Na Joachim Nyambo,Mbarali.

WAJAWAZITO kusafirishwa kwa Bodaboda na Powertiller kutoka kijijini kwao kwaajili ya kwenda kujifungua wanapopatwa na uchungu hadi mahali wanapoweza kupata huduma stahiki kumesababisha Baraza la wazee wa kata ya Kongolo wilayani Mbarali kupaza sauti zao wakitaka kuendelezwa kwa mradi wa ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Azimio mswiswi uliokwama tangu mwaka 2014.

Kwa mujibu wa uongozi wa kijiji cha Azimio Mswiswi mradi wa ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho uliibuliwa na wananchi ambao waliandelea na ujenzi wa jengo kuu hadi hatua ya kupaua lakini mara tu baada yam bio za mwenge wa Uhuru mwaka 2014 ambapo kiongozi wa Mwenge mwaka huo Rachel Kasanda kuweka jiwe la msingi kwenye jengo hilo ikawa mwisho wa mwendelezo wake.

Kutokana na kukosekana kwa zahanati kijijini hapo wakazi wameendelea kulazimika kutembea umbali mrefu hadi kijiji cha Kongolo Mkola kufuata huduma za matibabu ambapo hulazimika kutumia gharama kusafiri kwenda na kurudi.

Wajawazito kijijini hapo wanatajwa kuwa miongoni mwa wahanga wakubwa wa kadhia hiyo kwakuwa kutokana na kutokuwepo kwa usafiri wa gari wanapohitaji huduma ya matibabu ikiwemo huduma salama ya kujifungua wanapofikwa na uchungu hulazimika kusafirishwa kwa usafiri wa bodaboda au Trekta ndogo maarufu kama Powertiller huku barabara nayo ikiwa si rafiki hususani nyakati za masika.

Mwenyekiti wa kijiji cha Azimio Mswiswi,Aliagiza Ngwipa alisema mradi huo ulianza kutekelezwa kwa nguvu ya wananchi toka mwaka 2013 lakini ulitelekezwa toka siku ulipowekewaa jiwe la msingi katika mbio za Mwenge wa uhuru mwaka 2014.

Ngwipa alikiri kuwa kutokamilika kwa mradi huo kumewafanya wakazi hususani wajawazito na wazee kupata wakati mgumu kusafiri kufuata matibabu hatua iliyowafanya wapaze sauti zao na kutaka kujua nini mpango wa Serikali katika kukamilisha ujenzi huo ili waanze kupata matibabu jirani.

Alisema kwa sasa wakazi wa kijiji hicho wanalazimika kutembea umbali wa zaidi ya Kilometa tano kufuata matibabu katika Zahanati ya kijiji cha Kongolo Mkola ambacho ndicho pekee kina zahanati katika vijiji vyote vitano vinavyounda kata hiyo.

Aliongeza kuwa kama uongozi wa kijiji wamefuatilia Halmashauri kujua hatma ya jengo lao baada ya kuona linaanza kuchakaa likiwa limeezekwa na kuwekwa milango na kilichosalia ilikuwa uwekaji wa madirisha,kusakafia na kupiga sealingboard.

“Tumefuatilia sana baadaye uongozi wa wilaya umetuagiza tujenge kwanza choo..tunaendelea kujichangisha wanakijiji mpaka ujenzi wa choo umefikia hapa tulipo.Kwa tathmini ya watu wa wilayani walisema gharama ya choo inaweza kawa milioni tano.Kwa upande wa jengo mafundi wetu wamefanya tathmini wamesema karibia Milioni 10 zinaweza kukamilisha kazi zilizosalia ili jengo liweze kufanya kazi.”  Alisema

 

“Sera ya Serikali inasema kila kijiji kiwe na zahanati na kila kata kituo cha afya lakini huku kwetu haijatekelezwa.Pamoja na jitihada zilizofanywa na wananchi kuanzisha ujenzi.Halmashauri baadaye ilichangia fedha kidogo lakini baada ya kuweka jiwe la msingi kukawa kimya.Tunasubiri baada ya kujenga choo wanakijiji tuone mkono wa Serikali na sisi ili tupate matibabu stahiki.Vipo vitongoji vingi vya wafuagi ambavyo vipo mbali zaidi ya hapa tulipo ambavyo watu wake wangerahisishiwa kwa kupata matibabu hapa.” Aliongeza mwenyekiti huyo.

Baraza la wazee linasema linasikitishwa zaidi linaposikia jitihada zinazofanywa na wananchi na wadau kwenye maeneo mbalimbali ambazo wanasikia kwenye vyombo vya habari nchini kuwa zinaungwa mkono na Serikali na hatimaye wananchi hususani wajawazito na wazee kuanza kunufaika na miradi ya huduma za afya jirani na kuhoji kwa nini kwenye kata yao isiwezekane.

Katibu wa Baraza la Wazee wilaya ya Mbarali,Ezron Kapwela alisema imefika wakati wadau kuhakikisha ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho unakamilika ili kuepusha pia vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga wanaohitaji huduma rafiki wakati wa kujifungua na kuzaliwa.

“Tunaona na kusikia kila siku kupitia vyombo vya habari kulee mradi umekamilika….kuleee mradi wananchi wameibua Serikali imewasaidia umeanza kutoa huduma..sijui wapi wajawazito sasa wameacha kutembea umbali mrefu…na maeneo mengine ni ya hapahapa mkoani kwetu Mbeya..sasa tunajiuliza hivi sisi tunashindwa wapi?.Hatuwezi kulifumbia macho jambo hili maana wakati wa mvua nyingi barabara pia huku kwenye maeneo mengi ya kata yetu hayapitiki kwakuwa maji yanatapakaa na hauwezi kujua barabara iko wapi” alisema Kapwela.

Mkazi wa kijiji hicho Mary Kyando anasema “Miaka yote zahanati haiishi..wagonjwa wanafia njiani..mtoto anashikwa na uchungu hapa anabebwaje kwenye bodaboda mpaka kule zahanati iliko..yaani anafungwa minati kwenye bodaboda utafikiri mzigo wa kuni.Tunataka tuone matunda ya michango yetu.”

Akimwakilisha mganga mkuu wa mkoa wa Mbeya kwenye,Afisa kutoka Ofisi hiyo,Dk Peter Mereki aliwapongeza wakazi wa kijiji hicho kwa kuchukua uamuzi wa kuanzisha mradi na kuwahakikishia kuwa Serikali haiwezi kuacha mchango wao ukapotea bure bali jitihada za dhati zitafanyika ili kuikamilisha zahanati ianze kutoa huduma.

Dk Mereki aliitaja kata ya Kongoro kuwa miongoni mwa maeneo mkoani hapa yaliyo na mwamko mkubwa katika kujiunga na Bima ya Afya hivyo ni muhimu wakazi wake wakajengewa mazingira ya kupata huduma za afya kwa karibu ili wafaidi matunda ya mwamko wao.

Aliwataka wakazi wa vijiji vingine vya kata hiyo kuiga mfano wa wenzao wa Azimio Mswiswi kwa kuanzisha ujenzi wa zahanati wao wenyewe badala ya kusubiri mpaka Serikali ikawaanzishie hatua aliyosema inaweza kuwachelewesha zaidi.

“Hatukuja hapa kwaajili ya kuona tu..Yote mliyoyafanya tumeyaelewa na kuyathamini.Huduma za matibabu tunaendelea kuboresha siku hadi siku.Suala la milioni 10 za kumalizia jengo nitaliwasilisha kwa uzito wake.Ninyi mmejitambua mmeitambua mpaka Sera.Na mmejitolea bado choo tu ambacho nacho mmefikia hatua nzuri.Vijiji vingine navyo viige mfano wenu.”alihimiza Dk Mereki.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post