WANANCHI ARUSHA WAPUUZA MATUMIZI YA VIFAA VYA KUJIKINGA NA CORONA

Na Claud Gwandu, Arusha  

LICHA ya Serikali kuendelea kutoa elimu ya matumizi sahihi ya vifaa vya kujikinga na maaambukizi ya virusi vya corona bado baadhi ya wananchi Jiji la Arusha wamekuwa wakipuuza zoezi hilo.

 

Wakizungumza na blog hii baadhi ya wananchi katika jiji la Arusha wamesema kuwa jamii imekuwa ikipuuza uvaaji sahihi wa vifaa vya kujikinga na corona   ikiwemo kuvaa barakoa kwa siku tatu bila kuifua jambo linaloweza kuhatarisha maambukizi mapya.

 

Wananchi hao walisema kuwa wanapaswa kuendelea kutumia vizuri vifaa hivyo vya kujikinga dhidi ya virusi vya ugonjwa wa Corona ili kuweza kuweka jamii katika sehemu salama zaidi.

 

"Wananchi wengi hivi sasa wameacha kunawa mikono au kutakasa mikono yao Kutokana na kuamini kuwa ugonjwa huo umeisha jambo ambalo sio sahihi kutokana na Corona kuwepo kwenye nchi za jirani jambo ambalo linasisitizwa na serikali kuendelea kujinga na Corona"walisema

 

Walisema baadhi ya wananchi wamekuwa wakivaa barakoa zaidi ya masaa matatu au wakivaa barakoa hizo tofauti na maelekezo sahihi ya kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Corona kama yanavyoelekezwa na taasisi za afya.

 

Paul Loishiye anayejitambulisha kama mdau wa masuala ya Afya  mkoani Arusha alisema kuwa wananchi wanapaswa kuendelea kusikiliza vyombo mbalimbali vya habari ili kujua nini kinaendelea na kupata elimu ya virusi vya Corona kutoka katika taasisi za kiserikali na taasisi nyingine. 

 

Naye Dkt. Innocent Lyamuya mdau wa masuala ya Afya mkoani Arusha  aliishauri jamii kuendelea kufuata ushauri uliowekwa na wataalamu wa afya ikiwemo kutumia barakoa kwa usahihi pamoja na kutumia vitakasa mikono ili kujikinga na corona.

 

Dkt Lyamuya ambaye ni mfanyakazi katika hospitali ya rufaa ya ALMC Jijini Arusha amesema wamekuwa wakitoa elimu kwa wananchi ya kujikinga na Corona huku akiwataka wananchi kuendelea kuzingatia usafi.

 

“Sisi ukija hospitalini lazima uvae barakoa kwaajili ya kujikinga na maradhi ya corona, ijapokuwa Tanzania ugonjwa umeisha lakini ni lazima watu wajikinge na wafanye kuvaa vifaa hivyo ni kama utamaduni, huwezi kujua ugonjwa utaibuka lini tena,”alisema.

 

Alisema kuwa wananchi wanatakiwa kuendelea kuzingatia kufanya usafi na kuwa wasafi muda wote  na kwamba hiyo ndio njia sahihi kuepukana na maambukizi ya virusi vya Corona. 

 

David alisema wamekua wakitoa elimu mara kwa mara kwa viongozi mbalimbali juu ya kujikinga dhidi ya virusi vya Corona hasa katika yote ya umma 

 
Serikali kupitia Wizara ya Afya maendeleo ya Jamii jinsia wazee na watoto imesema kuwa ili kukabiliana na maambukizi ya Corona ni vyema wananchi wakaepukana na mikusanyiko isiyokuwa na lazima, kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa maji Tiririka na sabuni pamoja na kutumia vitakasa mikono.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post