Na Dismas Lyassa, Kibaha Mjini
“NAAGIZA TAKUKURU fuatilieni suala la migogoro ya ardhi,” ni kauli ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya Kibaha Mjini, Maulid Bundala alipofanya ziara kutembelea Mtaa wa Vikawe kwa lengo la kuzungumza na viongozi na wananchi kuhusu migogoro ya ardhi inayoendelea katika eneo hilo.
Ziara hiyo ambayo ilishirikisha wajumbe wa Kamati ya siasa CCM Wilaya Kibaha Mjini ilifanyika kufuatilia hivi karibuni wananchi kufunga ofisi ya Serikali ya Mtaa kutokana na mgogoro wa ardhi baina ya wananchi na viongozi wao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi wameshauri vyombo vya dola kufanya uchunguzi kwa kuwatambua wanaoendeleza utapeli wa viwanja katika Kata Pangani na kuchukua hatua kwani baadhi yao wanadaiwa kuwa ni viongozi.
“Ukweli ndugu mwandishi, migogoro ya ardhi ina athari kubwa sana kwa jamii, unakuta mtu anajenga nyumba halafu anaambiwa hiki kiwanja sio chako… mambo kama haya ni ya kawaida sana katika Kata hii ya Pangani, bahati mbaya sana wanaofanya utapeli wanafahamika, inadaiwa hawachukuliwi hatua kwa sababu ni mtandao unaonufaisha hadi baadhi ya wakubwa juu, wanatumia rushwa na wengine wanakesha kwa waganga kutafuta dawa za kutapeli watu ardhi,” alisema mkazi mmoja wa Vikawe Shuleni ambaye hakupenda jina lake litajwe.
Kwa upande wake Bi. Zamda Komba, ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa CCM Wilaya Kibaha Mjini alisema Pangani ndio kata inayoongoza kwa migogoro ya ardhi katika wilaya nzima ya Kibaha Mjini, sifa ambayo sio nzuri, hivyo akashauri jitihada zifanywe kuondokana na sifa hiyo mbaya.
Hata hivyo baadhi ya wananchi wana hofu kama sifa hii inaweza kuondoka Kata Pangani wakidai vinara wakuu wa utapeli wa ardhi ni baadhi ya viongozi, ambao wengine wanahusika moja kwa moja kuuza hadi ardhi ya Mitamba ambalo ni mali ya Serikali, ilikuwa inatumika kulishia mifugo ambalo sasa halitumiki. Baadhi ya viongozi wanadaiwa kujikatia ardhi watakavyo katika ardhi hiyo ya Serikali wakitumia majina jamaa zao. Aidha baadhi ya viongozi ambao ndio walipaswa kuwa kimbilio la wananchi wasitapeliwe tayari wana kesi walizofunguliwa na wananchi wakiwatuhumu kuchukua ardhi zao.
Mwisho