Afisa Udhibiti Ubora TBS, Bw.Diocles Ntamulyango akizungumza na Waandishi wa habari katika ofisi za TBS leo Jijini Dar es Salaam.
Katika zoezi la Ukaguzi wa Magari bandarini, mpaka sasa TBS imeshakagua magari 5,445 na kati ya hayo magari 2367 yalibainika na kasoro zinazotengenezeka.
Ameyasema hayo leo Afisa Udhibiti Ubora wa Shirika la Viwango Tanzania TBS, Bw.Diocles Ntamulyango katika ofisi za shirika hilo Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi hizo, Bw.Ntamulyango amesema katika magari ambayo yamebainika na kasoro kati ya hayo magari 1567 yamekwisha rekebishwa na kupimwa upya na yamekidhi matakwa ya viwango na yamesharuhusiwa kusajiliwa na TRA.
"Mpaka sasa tuna mashine tano ambazo zinatumika katika kukagua magari ambapo mashine nne zipo katika kituo cha TPA na mashine moja ipo katika kituo cha UDA". Amesema Bw.Ntamulyango.
Aidha Bw.Ntamulyango amesema mashine nne za kukagua magari zinauwezo wa kupima magari 496 kwa siku hivyo wanauwezo wa kupima zaidi ya magari 14,000 kwa mwezi.
Hata hivyo Bw.Ntamulyango amesema upimaji wa magari unafanyika katika vituo viwili, kituo cha kwanza kipo ndani ya bandari kipo karibu na Roro yard na kituo cha pili kipo maeneo ya UDA.