Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, Mkoa wa Morogoro, Juni 17, 2021. Hafla hiyo ilifanyika kijiji cha Muheza Ititu Wilaya ya Gairo.
*Mbunge wa Kilosa ambaye pia ni Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, Mkoa wa Morogoro. Uzinduzi huo ulifanyika katika kijiji cha Muheza Ititu wilayani Gairo, Juni 17, 2021.
Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, Mkoa wa Morogoro. Uzinduzi huo ulifanyika katika kijiji cha Muheza Ititu wilayani Gairo Juni 17, 2021.
Mbunge wa Morogoro Kusini, Innocent Kalogeris akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, Mkoa wa Morogoro. Uzinduzi huo ulifanyika katika kijiji cha Muheza Ititu, Juni 17, 2021.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martin Shigela akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, Mkoa wa Morogoro. Uzinduzi huo ulifanyika katika kijiji cha Muheza Ititu, wilayani Gairo Juni 17, 2021.
Mbunge wa Jimbo la Mikumi, Dennis Londo akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, Mkoa wa Morogoro. Uzinduzi huo ulifanyika katika kijiji cha Muheza Ititu wilayani Gairo, Juni 17, 2021.
Wananchi wakiwa katika hafla ya uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, Mkoa wa Morogoro. Uzinduzi huo ulifanyika katika kijiji cha Muheza Ititu wilayani Gairo, Juni 17, 2021
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Elineema Mkumbo akipunga mkono kuwasalimu wananchi wa Gairo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, Mkoa wa Morogoro. Uzinduzi huo uliofanyika Juni 17, 2021 katika kijiji cha Muheza Ititu wilayani Gairo. Kulia kwake ni Mjumbe wa Bodi ya Wakala huo, Florian Haule.
Na Veronica Simba - REA
Viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Morogoro hususani Wabunge wameipongeza Serikali kwa utekelezaji mzuri wa Miradi ya Umeme Vijijini.
Walitoa pongezi hizo kwa nyakati tofauti jana, Juni 17, 2021 wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili katika Mkoa wa Morogoro, uliofanyika kijiji cha Muheza Ititu, wilayani Gairo.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, Mkuu wa Mkoa huo, Martin Shigela alitoa pongezi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake mzuri uliowezesha sekta mbalimbali nchini ikiwemo ya nishati kuendelea kufanya vizuri.
Akifafanua, alisema kuwa alipokabidhiwa Ofisi Machi 15 mwaka huu, idadi ya vijiji vilivyokuwa na umeme mkoani humo ni 433 na kuongeza kuwa amefarijika kuona Waziri Kalemani ameenda kuwakabidhi rasmi Wakandarasi kwa ajili ya kumalizia vijiji 235 vilivyobaki.
"Mheshimiwa Waziri, tufikishie shukrani zetu kwa Mheshimiwa Rais na tunamwahidi kuwa umeme huu unaenda kuleta tija kwa maisha ya wananchi wa Morogoro."
RC Shigela alisema kuwa wananchi wa Morogoro watautumia umeme huo pamoja na mambo mengine kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ambayo wanazalisha kwa wingi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kilosa ambaye pia ni Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi alibainisha kuwa alipochaguliwa kuwa Mbunge, alikuwa akilionea wivu jimbo la Gairo kutokana na kuwa na vijiji vingi zaidi vyenye umeme, lakini sasa anafarijika kuona kwamba vijiji 63 vya jimbo lake vitapata umeme kupitia Mradi uliozinduliwa.
Haya ni mapinduzi makubwa ambayo tunajivunia sana, " alisema Prof. Kabudi.
Aidha, aliwataka Watanzania kujivunia mafanikio iliyopata katika usambazaji umeme vijijini kwani kwa sasa ndiyo kinara wa kupeleka umeme vijijini katika Bara la Afrika.
"Watanzania hatupendi kujisifia. Hizi siyo zama za kusubiri kusifiwa. Ukifanya jambo zuri usisubiri wakusifu. Jisifu mwenyewe. Na kwa hili tunastahili kujisifu, " alisema.
Naye Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby alibainisha kuwa kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Serikali, vijiji ambavyo havijapata umeme katika jimbo lake vimebaki saba tu na wakandarasi wanaendelea na kazi.
"Niwapongeze sana REA na TANESCO. Wamefanya kazi kubwa sana. Hata mimi mwenyewe na ubunge wangu huu, kuna baadhi ya maeneo sikuwahi kutegemea umeme utafika lakini umefika."
Mbunge wa Jimbo la Mikumi, Dennis Londo pamoja na kuipongeza Serikali, alisema kuwa anaamini uwepo wa umeme utawezesha mapinduzi katika sekta zote za uzalishaji na hivyo kuwawezesha wananchi kupambana na umaskini.
Mbunge wa Morogoro Kusini, Innocent Kalogeris alisema amefarijika kuona ahadi zilizoahidiwa na Chama chake (CCM) wakati wa kampeni zinaendelea kutekelezwa kwa kasi.
"Katika jimbo langu la Morogoro Kusini, vijiji ambavyo vinakwenda kupata umeme kupitia mradi huu ni 51. Huu ni ushindi mkubwa sana kwetu," alisema.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Kalemani alibainisha kuwa uzinduzi huo ni moja ya matukio ya mafanikio makubwa ya Serikali katika utekelezaji wa miradi ya kusambaza nishati vijijini kwani ni ukamilishaji wa ngwe ya mwisho ya kupeleka umeme katika vijiji vilivyosalia.
"Itakapofika Desemba 2022, Tanzania itaandika historia katika vitabu vyake kuwa vijiji vyote vya Tanzania Bara vimepata umeme.
Aidha, Waziri alibainisha kuwa Serikali imetenga takribani shilingi bilioni 66.8 kwa Mkoa wa Morogoro pekee ili kuhakikisha vijiji vyote 233 vilivyosalia bila umeme kati ya 673 vilivyopo, vinapatiwa nishati hiyo.
Hafla hiyo ya uzinduzi ilihudhuriwa na viongozi pamoja na wataalam wengine mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati, REA na TANESCO na wananchi.