WAKAZI WA KATA YA MARUVANGO WAAZIMIA KUMALIZA TATIZO LA UKATILI WA KINGONO.

Washiriki katika mdahalo kuhusu msaada wa kisheria kwa wahanga wa ukatili wa kingono Kata ya Maruvango.
Mwezeshaji katika mdahalo kuhusu msaada wa kisheria kwa wahanga wa ukatili wa kingono Kata ya Maruvango, Joyce Mwanga.
Mwezeshaji kwenye mdahalo kuhusu msaada wa kisheria kwa wahanga wa ukatili wa kingono Kata ya Maruvango, Evarester Mlamie.
Mwezeshaji kwenye mdahalo kuhusu msaada wa kisheria kwa wahanga wa ukatili wa kingono Kata ya Maruvango, Jackson Muro.
Washiriki wakiwa kwenye vikundi vya majadiliano kuhusu msaada wa kisheria kwa wahanga wa ukatili wa kingono Kata ya Maruvango.


Na Debora Robert, Meru.


Wananchi wa Kata ya Mavurango iliyopo wilaya ya Meru mkoani Arusha kwa pamoja wameazimia kuyafikisha katika vyombo vya maamuzi vya kisheria masuala yote yanayohusiana na ukatili wa kingono badala ya kuyamaliza kimila au kifamilia.


Hatua hiyo imekuja baada ya Shirika la Tusonge Community Development Organisation la Mjini Moshi kwa kushirikiana na mashirika ya Community Economic Development and Social Transformation (CEDESOTA),  Smart Community on Legal Protection, Women’s Economy and Gender Support (WEGS),Shirika la Deploy & Nurturing Gallery (DNG Tanzania), pamoja na wawezeshaji wengine wa kujitegemea kutoa elimu juu ya madhara ya ukatili wa kijinsia kwa jamii hiyo kwa muda wa miaka mitatu sasa.


Maazimio mengine ni kuvitaka vyombo vya dola kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaobainika kukataa kutoa ushahidi au kuharibu ushahidi kwenye masuala yanayohusiana na ukatili wa kingono pamoja na kuhakikisha kunakuwepo na ushirikianao wa karibu kati ya viongozi wa vitongoji, vijiji, Kata na wananchi katika kukomesha tabia hiyo.


Katika mdahalo huo uliolenga msaada wa kisheria kwa wahanga wa ukatili wa kingono kwa wananwake, wasichana na wavulana ulioandaliwa na mashirika hayo, wananchi hao wamesema wamekuwa wanapata changamoto ya huduma hiyo kutokana na kukosekana kwa askari Kata pamoja na Afisa Ustawi wa Jamii jambo linalochangia kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo.


Akichangia mdahalo huo uliowakutanisha viongozi wa serikali ngazi ya kitongoji hadi ngazi ya Kata, viongozi wa dini, viongozi wa mila, wanasiasa, wanajamii askari wa dawati la jinsia, Afisa Ustawi wa Jamii, Afisa Maendeleo ya Jamii wote kutoka wilayani hapo, Mkurugenzi wa Shirika la CEDESOTA, Jackson Muro amewataka viongozi hao kutoa elimu endelevu kwa jamii hiyo juu ya madhara ya ukatili wa kingono kwa wanawake, vijana na wasichana kwani hakuna mila, dini na hata jamii inayoruhusu maovu yakiwemo ya ubakaji.


“Mmesema wenyewe kuwa tatizo la ukatili wa kingono upo kwenye Kata hii, lakini pia mmesema hakuna huduma za kisheria kama polisi wala ustawi wa jamii, hivyo sisi kama wanaharakati tunashirikiana na serikali na ndiyo maana leo mmeona tumekuja na polisi dawati la jinsia, afisa ustawi wa jamii pamoja na afisa maendeleo ya jamii, lengo ni kuona ni jinsi gani tunatatua changamoto hii” Alisema Muro.


Mkurugenzi wa WEGS, Joyce Mwanga aliwataka washiriki hao kuwa mabalozi wazuri kwenye jamii zao ili kuhakikisha kila mmoja ni mlinzi wa mwenzake na iwapo itatokea tukio lolote la ukatili wa kingono basi jamii yote itoe ushirikiano kwa mamlaka husika pamoja na kuwashawishi wahanga wa matukio hao kupaza sauti zao ili haki itendeke na kukomesha vitendo hivyo viovu katika jamii.


“Kama mlivyosema kuwa elimu itolewe, lakini niwaambie kuwa kwa muda ambao tumekuwa tukitoa elimu kwa jamii hii juu ya madhara ya ukatili wa kingono na nini kifanyike, ni wakati sasa wa kuonyesha uelewa wenu kwa kuhakikisha hakuna vitendo hivi ndani ya Kata yenu, lakini hata ikitokea mhakikishe mhanga wa vitendo hivi hajifichi ndani, watoke mshirikiane kwa pamoja kupaza sauti ili haki itendeke, lakini viongozi pia mnatakiwa kuwa mstari wa mbele ikiwa ni pamoja na kuepukana na rushwa” Alisema Mama Mwanga.


Evarester Mlamie ambaye ni mwezeshaji katika mdahao huo alisema ni wakati sasa wa kuhakikisha Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) ambao umeandaliwa na serikali kwa ajili ya kuboresha utoaji huduma kwa makundi yaliyo katika mazingira haratishi unafanya kazi kwani itasaidia kuwalinda wanawake, wasichana na wavulana dhidi ya ukatili wa kingono.


Mtendaji wa Kata hiyo Longumo Sabore amewaambia wananchi hao kuwa ni kweli Kata hiyo ilikuwa haina askari wa Kata lakini kwa sasa yupo amesharipo kituo cha kazi muda si mrefu na kwamba changamoto ya kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kwenda kituo cha polisi imetatuliwa kwani masuala yote yanayohusu jinai yakiwemo ukatili wa kingono yataripotiwa kwa wakati.


Naye Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka halmashauri ya wilaya ya Meru Flora Msilu amesema kutokana na changamoto alizosikia ameahidi kuanzia mwezi Juni mwaka huu kumpelekea afisa maendeleo ya jamii kwenye Kata hiyo ili afanye kazi za afisa ustawi wa jamii lengo ni kusogeza huduma karibu na kijamii.


Polisi kutoka dawati wa jinsia wilaya ya Meru, Salama Ally amewataka wanajamii hao kutoa taarifa polisi kwa wakati ikiwa ni pamoja kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi pamoja na mahakama wakati wanaposhughulikia kesi hizo ili kuwabaini wahalifu hao kwa lengo la  kukomesha vitendo hivyo.


Awali wananchi waliochangia katika mdahalo huo Elizabeth Senyael, Malaki Akyoo, Bertha Mbise na William Mafie walisema baadhi ya wazazi wamekuwa na tabia ya kuwaficha wahanga wa vitendo hivyo hususani wasichana wajawazito kwa madai kuwa kutoa taarifa kwa jamii au vyombo vya dola itapelekea mhanga huyo kuchukua maamuzi mabaya ikiwemo kujitoa uhali kwa kuona amedhalilishwa kwenye jamii.


Naye Diwani wa Kata hiyo Godson Majola amesema yote yalizungumzwa na kuazimiwa yatafanyiwa kazi kwa kushirikiana na jamii na serikali na kwamba atahakikisha tabia ya kuwaficha wahanga na wahalifu inakomeshwa ili kuhakikisha makundi hayo yanaishi kwa amani ndani ya jamii.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post