DC MTANDA ATAKA SHERIA YA KUWANYIMA DHAMANA WATUHUMIWA WA UBAKAJI, ULAWITI


Na Debora Robert,

Arusha.


Mkuu wa wilaya ya Arusha Said Mtanda ameliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutunga sheria itakayomnyima dhamana mtuhumiwa wa makosa ya ukatili yakiwemo ubakaji na ulawiti ili kukomesha vitendo hivyo katika jamii.


Mkuu wa wilaya ameyasema hayo jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika mjini hapa na kuomba bunge lipitie sheria iliyopo inayompa dhamana mtuhumiwa wa makosa hayo na kusema kama tuhuma za uhujumu uchumi pamoja na ugaidi hazina dhamana basi ni vyema hata kesi za uhujumu watoto zisiwe na dhamana kwani makosa hayo yanaathiri maisha ya watoto.


“Nasema haya nikiwa kama mdau wa haki za watoto, wabunge waone kuna haja ya kuangalia sheria hii, unakuta mtu anatuhumiwa kubaka watoto zaidi ya ishirini lakini anapewa dhamana, hata kama hajakutwa na hatia lakini ni vyema akawa ndani ili mwisho wa siku watu waogope kutenda matendo haya ya kinyama kwa watoto kwa kuhofia sheria kali iliyopo” Alisema Mtanda.


Mtanda amesema nia ya kuomba sheria hiyo irekebishwe ni ili kuweka mazingira salama kwa watoto kwa lengo la kutengeneza Taifa bora la baadaye kwani watoto waliofanyiwa ukatili mara nyingi hukata tamaa ya maisha kutokana na msongo wa mawazo na hata kujiingiza kwenye matumizi wa dawa za kulevya. 


Kwa upande mwingine Mkuu huyo wa Wilaya amepiga marufuku na kutoa onyo kali kwa walimu wa shule za msingi na sekondari wenye tabia za kuwarudisha wanafunzi majumbani kwa sababu ya kutolipa michango mbalimbali na kuongeza michango yote ni lazima ipate baraka zake kabla ya utekelezaji wake.


“Nilishawahi kusema na leo narudia tena, hakuna mwanafunzi wa shule ya msingi wala sekondari kurudishwa shule kwa sababu ya kutolipa mchongo wowote, hilo ni kosa la mzazi, mkuu wa shule tafuta mgambo aende kumkata mzazi wa mwanafunzi” Alisema na kuongeza.


“Kwanza michango yote ipitie kwenye kamati ya wazazi, muhtasari upelekwe kwa Mkurugenzi halafu uje kwangu mkuu wa wilaya, niupitie niridhike ndiyo utumike, kwa sababu  kuna baadhi ya shule zina michango ya hovyo kwa mfano mchango wa rimu, mchango wa Jumamosi, mchango wa mlinzi nk, wakati Rais ameshasema elimu bure lakini bado kuna michango ya hovyo”


Akitoa mada juu ya ukatili kwa watoto, Afisa Ustawi wa Jamii Jiji la Arusha Nivo Kikaho amewataka watoto kuwa makini na kujilinda kwa kuhakikisha kuwa wanapita sehemu salama wakati wote wanapokuwa mbali na majumbani mwao ikiwa ni pamoja na kuacha tabia ya kuzoea watu wasio wafahamu.


“Lakini pia mnatakiwa kuheshimu wazazi na watu wazima. mkiwa na heshima ni rahisi sana kuepuka vitendo vya kikatili, msizurure mitaani, mkitoka shule muende moja kwa moja nyumbani msipite sehemu yoyote lakini pia usiruhusu mtu yeyote kushika mwili wako, iwapo itatokea kitendo hicho piga kelele ili upate msaada” Alisema Kikaho.


Wakisoma risala kwa mgeni Rasmi, watoto hao wameiomba Serikali pamoja na wadau wa maendeleo ya watoto wakiwemo mahakama, baraza ya watoto, taasisi za ulinzi na wazazi, kukaa pamoja na kutafakari mbinu za kukomesha vitendo vinavyowaathiri kimwili na kiafya na kushindwa kuyafikia malengo yao ya kulijenga Taifa bora la Tanzania.


Maadhimisho ya mtoto wa Afrika wilaya ya Arusha yalihudhuriwa na wanafunzi kutoka shule mbalimbali za msingi na sekondari wilayani humo ambapo walipendezesha siku yao kwa kutoa burudani mbalimbali zikiwemo sarakasi, nyimbo pamoja na ngonjera huku kauli mbiu ikisema “Tuimarishe Ulinzi wa Mtoto, Tokomeza Ukatili Dhidi ya Mtoto, Jiandae Kuhesabiwa”.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post