MFANYABIASHARA SINGIDA ADAIWA KUMTEKA MFANYAKAZI WAKE KWA MIAKA 10 NA KUPORA NYUMBA

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Binilith Mahenge

 Na Dotto Mwaibale, Singida

MFANYABIASHARA mmoja maarufu wa mjini Singida mkoani hapa anadaiwa kumteka na kumficha kusikojulikana kwa zaidi ya miaka 10 sasa mtu mmoja aliyekuwa mfanyakazi wake na haijulikani kama yupo hai au amefariki.

Madai hayo yalitolewa na Omari Rashid juzi mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk.Binilith Mahenge, kwenye mkutano wa kusikiliza kero za wananchi uliofanyika katika viwanja vya  Stendi ya Zamani Manispaa ya Singida.

Rashid ambaye alidai ni mtoto wa mtu huyo aliyetekwa, alieleza kuwa baba yao  hajaonekana tangu mwaka 2010 baada ya mfanyabiashara huyo kumlaghai na kuchukua hati ya nyumba yao na kisha kuwafukuza katika nyumba hiyo ambapo sasa wanaishi kwa kutangatanga.

Aliongeza kuwa mfanyabiashara huyo (anamtaja jina) alimrubuni baba yao kwamba atamlea na familia yake kwa kipindi chote cha maisha yao lakini katika hali ya kushangaza wamejikuta wakitimuliwa na mfanyabiashara huyo ambaye amejimilikisha nyumba yao iliyopo eneo la Majengo Manispaa ya Singida.

Rashid alisema kinachowashanga na kujiuliza maswali yasiyo na majibu ni kwamba baba yao hajaonekana tangu mwaka huo hali inayowafanya waingiwe na hofu kama yupo hai au amekufa.

"Mheshimiwa RC utatusaidiaje jambo hili ili tupate nyumba yetu na tujue hatma ya baba yetu alipo," alisema.

Kufuatia ombi hilo, Mkuu wa Mkoa Singida, Dk.Mahenge alimwagiza Katibu Tawala wa Wilaya ya Singida ( DAS) na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Lucas Mwakatundu wachukue maelezo ya kina ya mlalamikaji huyo ili serikali iweze kuyafanyia kazi madai yake.

Aidha, Dk.Mahenge aliwagiza viongozi kuanzia ngazi za wilaya hadi chini kujenga tabia ya kuitisha mikutano ya wananchi na kusikiliza kero zao.

 Alitumia nafasi hiyo kuwaeleza wananchi mafanikio mbalimbali yaliyofanywa na serikali ya awamu sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Mkuu huyo wa mkoa alisema katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan  Mkoa wa Singida umepatiwa Sh.Bilioni 230 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji, Barabara, Elimu, Umeme na ya Sekta ya Afya.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post