Halmashauri ya Mji Babati katika kashfa ya rushwa

Ofisi za Halmashauri ya Mji Babati ( Picha na mtandao)

 *Askari wake wa ukaguzi wadaiwa kudai ushuru wa mazao mafuta yaliyokamuliwa

*Wadanganya wafanyabiashara ni kodi mpya iliyopitishwa na bunge la bajeti


Na Seif Mangwangi, Arusha


Halmashauri ya Mji wa Babati Mkoani Manyara imeingia katika kashfa baada ya wafanyakazi wake kudaiwa kuanzisha mtindo wa kudai rushwa wafanyabiashara kwa kisingizio cha sheria mpya iliyopitishwa na Bunge la bajeti mwezi Juni 2022 ambayo si kweli.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti wafanyabishara hao wamesema tatizo hilo limejitokeza katika kituo cha ukaguzi kilichopo katika eneo la Ango barabara kuu ya Babati, Arusha.


Wamesema askari hao wa Halmashauri husimamisha magari yaliyobeba bidhaa hususani mafuta ya kula ya alizeti na kuwalazimisha  wasafirishaji wa bidhaa hiyo kuilipia ushuru wa Tsh500 kwa kila dumu.


Abdallah Ramadhani ni mfanyabiashara wa bidhaa ya mafuta ya kula aina ya alizeti ambaye anasema juzi akiwa njiani kusafirisha bidhaa yake akitokea Mkoani Singida alikutana na mkasa huo na kushindwa kuelewa ushuru huo unatokana na sheria gani.


" Mimi juzi nilifika Babati saa3 usiku, nikiwa nimepakiza dumu 900 za mafuta ya alizeti, nilipofika pale Ango kwenye kituo cha ukaguzi wa mazao nilisimamishwa nikaanza kukaguliwa, hata hivyo niliwaeleza nimebeba mafuta ya kula wakasema natakiwa kulipia ushuru wa Tsh500 kwa kila dumu la lita20 nililokuwa nimepakiza," anasema Abdallah na kuongeza: 


" Nilihoji huo ushuru ni kwaajili ya nini wakaniambia ni ushuru wa Halmashauri na umeanza mwezi wa saba baada ya sheria mpya kupitishwa, nikamwambia mimi sijui hiyo sheria lakini mzigo wetu tumeshaulipia TRA bado walikataa kutuachia tuondoe, tulikaa pale hadi saa 8 usiku ndipo wakaturuhusu tuondoke, baada ya kuona tumegoma kabisa kutoa pesa," anasema


Anasema kutokana na shehena ya mzigo aliokuwa amepakia katika gari yake alipaswa kuwalipa askari hao Tshs 450,000 fedha ambayo haiko kisheria na hata alipowaeleza kuwa endapo wataendelea kung'ang'ania walipwe pesa hiyo itawabidi waikatie risiti waligoma.


Aidha anasema kwa kuwa yeye ni mzoefu katika barabara hiyo akitumia kusafirisha mafuta, mtindo huo wa kudaiwa ushuru kwenye bidhaa kutoka kiwandani ameweza kugundua kuwepo nyakati za usiku pekee jambo ambalo linaonyesha kubwa hiyo ni njia ya askari hao kutaka kujipatia rushwa kutoka kwa wafanyabishara.


Akizungumzia suala hilo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Babati, Anna Fissoo amesema hafahamu jambo hilo kwa kuwa ndio kwanza anapata taarifa na kuahidi kulifuatilia na baadae kulitokea ufafanuzi.

" Naomba unipatie muda nitakurejea, kwa kuwa jambo lenyewe ni yenu kwangu na hapa Babati nina vituo vya ukaguzi tofauti, ngoja nifuatilie," alisema Mkurugenzi huyo. 


Kutokana na suala hilo wafanyabiashara hao wameiomba Serikali hususani taasisi ya kupambana na kuzuia rushwa nchini (Takukuru), kufuatilia vituo vya ukaguzi wa mazao ili kuwanasa wafanyakazi wasiokuwa waadilifu wanaoendesha vitendo vya rushwa na kuumiza wafanyabiashara.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post