Russia yatishia kusimamisha uuzaji wa mafuta yake nje ya nchi

Russia imetishia kuwa itaacha kuuza mafuta yake ghafi nje ya nchi hiyo iwapo nchi za Magharibi zitatekeleza mpango wao wa kuweka kibano katika bei ya mauzo ya bidhaa hiyo.

Indhari hiyo imetolewa leo Alkhamisi na Alexander Novak, Naibu Waziri Mkuu wa Russia, ambaye amenukuliwa na shirika la habari la TASS akisema kuwa, iwapo bei ya mafuta itakayopendekezwa na Wamagharibi itaipelekea Russia isipate faida yoyote, basi hawatakuwa na budi kuacha kuzalisha bidhaa hiyo.

Ameeleza kuwa: Kama bei wazozungumzia zitakuwa chini ikilinganishwa na gharama za uzalishaji, bila shaka Russia itaacha kupeleka bidhaa hiyo kwenye soko la dunia, kwa kuwa hatuwezi kufanya biashara isiyo na faida.

Hivi karibuni, Kundi la G7 la mataifa saba yaliyostawi kiviwanda lilisema litaweka kibano kwenye bei ya mafuta ya Russia, kufikia mwishoni mwa mwezi Juni. Pendekezo hilo lilitolewa na Marekani ikidai kuwa, mpango huo utapelekea kupungua kwa mapato ya Russia kutoka na mauzo ya mafuta yake ghafi katika soko la dunia.


Nchi za Ulaya pamoja na makelele mengi ya vikwazo na vitisho dhidi ya Russia, lakini zinasuasua kutekeleza mpango huo kwa kuzingatia kuwa, zinategemea pakubwa mafuta na gesi kutoka Russia.

Hivi karibuni, Dmitry Medvedev, Mkuu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia alionya kuwa, iwapo Magharibi itatekeleza mpango huo wa kuweka kibano kwenye bei ya mafuta ya Russia, basi huenda bei ya bidhaa hiyo katika soko la kimataifa ikaongezeka na kufikia dola 300 hadi 400 za Marekani kwa pipa.

 

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post