Naibu waziri Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Omari Kipanga akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wenye uhitaji maalum katika sekondari mpya jumuishi ya Patandi ambayo aliizindua |
Naibu WAZIRI Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia Omar Kipanga akikataa utepe kuzindua sekondari jumuishi ya Patandi ambayo ni sekondari pekee ya mfano Tanzania yenye viwango vya Kimataifa |
Na Seif Mangwangi, Arusha
Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha sekta ya elimu nchini baada ya leo Julai 4, 2022 Naibu Waziri Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Omari Kipanga kuzindua shule Jumuishi ya mfano ya sekondari Patandi na ya kwanza kujengwa nchini kwaajili ya watoto wenye ulemavu na uhitaji Maalum.
Akizungumza katika uzinduzi wa shule hiyo Naibu Waziri Kipanga amesema Rais Samia anawapenda sana walemavu na ameshakutana nao mara kwa mara na kufanya mazungumzo ikiwemo kula nao chakula na sasa ameamua kujenga shule hiyo maalum.
Waziri Kipanga amesema katika kuendeleza elimu jumuishi nchini, Serikali imeondoa vikwazo vyote vya kielimu na kuhakikisha wanafunzi wote wanasoma pamoja bila kuwatenganisha.
"Serikali imewezesha ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya watoto wenye uhitaji Maalum, ununuzi wa vifaa kama bajaji, wheel chair, kuwajengea uwezo walimu 1700 wanaofundisha watoto maalum, lakini pia kuandaa kamusi ya watoto wenye uhitaji maalum,"amesema.
Amesema shule inayozinduliwa leo ni miongoni mwao mikakati ya Serikali ya ujenzi wa shule jumuishi na kuwaondolea watoto changamoto mbalimbali zilizokuwepo hapo mwanzo.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa shule hiyo Mkurugenzi wa elimu maalum kutoka wizara ya Elimu, Sayansi na teknolojia Dkt Magreth Matonya amesema shule hiyo iliyopewa jina la Shule ya Sekondari Maalum Patandi ilianza kujengwa mwaka 2017 na ni shule jumuishi kwa watoto wote.
Amesema ujenzi wa shule hiyo ambao umejumuisha madarasa ya kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne, maabara, jengo la utawala na Uzio imegharimu bilioni 3.835 hadi kukamilika kwake.
Amesema tangu shule hiyo ilipokamilika imeshapokea wanafunzi 288 ambao ni kuanzia kidato cha kwanza hadi cha tatu ikijumuisha watoto wenye ulemavu wa aina tofauti,na wenye mahitaji maalum.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu,Sayansi na teknolojia Prf Carolyne Ndosi amewataka wazazi wote nchini kuacha kuficha watoto wao nyumbani na badala yake wapeleke watoto wao katika sekondari jumuishi ya mfano Patandi kwa kuwa imejengwa kwa viwango vya hali ya kimataifa.
"Hii ni shule ya mfano wa kuigwa, ndio shule ya kwanza kujengwa Tanzania, inajumuisha watoto wa kawaida, watoto wenye ulemavu na uhitaji maalum na hasa wenye ulemavu wa kusikia,"amesema.
Amesema wizara yake imekuwa ikipokea maombi mengi kuhusu ujenzi wa shule ya namna hiyo hivyo wizara itaendelea kutafuta fedha ili kujenga shule zingine zitakazofanya na shule hiyo.
Naibu Katibu Mkuu Tamisemi Charles Msonde amesema itapendeza endapo shule zingine nzuri kama hiyo zitajengwa katika kanda mbalimbali za nchi ili kuondolea usumbufu wanafunzi wenye uhitaji maalum.