Na Seif Mangwangi, Arusha
MAMLAKA ya mapato nchini (TRA), imewataka waandishi wa habari kushirikiana na Mamlaka hiyo kubainisha wafanyabiashara wanaokwepa Kodi pamoja na watu wanaojifanya ni Watumishi wa TRA na kufanya utapeli kwa kuibia wafanyabiashara.
Wito huo umetolewa Jana Juni21,2023 Jijini hapa na Meneja wa Mamlaka ya Mapato Mkoa wa Arusha, Eva Raphael alipokuwa akifungua semina ya siku Moja kwa waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha kuhusu masuala ya Kodi.
Eva amesema Mamlaka hiyo imekuwa ikiandaa semina na warsha kwa makundi mbalimbali nchini ili kuwawezesha kujua umuhimu wa kulipa kodi kwaajili ya maendeleo ya nchi na kwamba bila Kodi mambo mengi yatakwama.
Amesema waandishi wa habari ni miongoni mwa makundi muhimu katika jamii ambayo yanatakiwa kupata elimu ya Kodi na kuitumia kuelimisha wananchi kwa kuwa vyombo vya habari ni rahisi kusambaza taarifa kwa haraka.
Amesema namba hiyo ni muhimu kwa kuwa hutumika kwenye huduma mbalimbali ikiwemo leseni za udereva na pia imekuwa ikionyesha uhalisia wa shughuli ambazo mtu binafsi amekuwa akizifanya.
" Na kwa kurahisisha zaidi TRA umeanza kutoa TIN kupitia njia ya mtandao, hii inasaidia kila mtu kupata TIN kwa urahisi na kwa wakati, sio TIN tu hata mnada wa magari na bidhaa mbalimbali zinazoshikiliwa na Mamlaka imekuwa ikifanyika online, wewe ingia tu kwenye mtandao wa TRA utaenda moja kwa moja kwenye kipengele cha Auction," amesema.
Afisa Uhusiano mwandamizi kutoka TRA makao Mkuu Rachel Mkunday amesema kila mwaka wa Serikali, bunge huchapisha kitabu Cha mwongozo wa Kodi ambacho hueleza sekta zinazopewa msamaha wa Kodi, kiwango cha Kodi kitakachotozwa kwa mwaka husika hivyo ni jukumu la Mamlaka hiyo kutoa elimu hiyo kwa jamii.
"Mfano kwa mwaka wa fedha unaoishia mwezi huu wa Juni 2023, Serikali ilitangaza kutoza Kodi ya asilimia 10 kwenye nyumba za biashara ambayo mpangaji anatakiwa kuikata wakati analipa Kodi yake ya pango, kuhusu nyumba binafsi za kupanga bado utaratibu haujawekwa na kwa mwaka huu wa fedha unaonda kuanza mwezi Julai bado wamepewa msamaha," amesema.
Amesema kuhusu Kodi ya majengo ambayo awali ilikuwa ikikusanywa kupitia mfumo wa Luku za Umeme, umehamishiwa Halmashauri ambazo zitatengeneza utaratibu wa kuzikusanya.
Amesema maendeleo ya nchi hujengwa na wananchi na waandishi wa habari ni sehemu ya kiungo muhimu kwa maendeleo hayo kwa kuwa ndio wamekuwa Karibu na jamii kutokana na taarifa zao ambazo huziripoti kila siku.
" Pamoja na kwamba Waandishi wa Habari wako Karibu na jamii, niwaombe TRA kuendesha semina kama hizi mara kwa mara waandishi wa habari ili kuwajenga uwezo katika uandishi wao, waandishi wakijua vizuri Kodi na wananchi watajua,"Amesema Gwandu.