Na Respice Swetu.
Wapenzi, mashabiki na wanachama wa timu ya Yanga wanaofanya kazi katika halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, wamefanya sherehe ya kuwapongeza wachezaji, viongozi na benchi la ufundi la timu ya Yanga kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika timu hiyo kwenye msimu wa ligi uliomalizika na mashindano ya Kimataifa.
Wakizungumza katika sherehe hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Villa Park mjini Kasulu wamesema, ushindi uliopatika kwenye mashindani ya ligi kuu na kitendo cha kufika fainali kwenye michuano mikubwa ya kombe la shirikisho barani Afrika, ni zawadi kubwa kwa wananchi na mashabiki wa timu hiyo.
Wamesema kuwa kutokana na mafanikio hayo, hakuna sababu kwa mashabiki, wapenzi na wanachama wa timu ya Yanga kuishi kinyonge kama ilivyo kwa mahasimu wao na ndio maana wakamuua kuandaa sherehe hiyo.
"Huu ni usiku wa mabingwa, tunakula, tunakunywa na kucheza tukiishangilia timu yetu ambayo pamoja na kufika katika hatua ya fainali kwenye mashindani yanayosimamiwa na shirikisho la soka la Afrika CAF, tumekuwa mabingwa wa ligi ya Tanzania kwa mara ya 29", alisikika mwananchi mmoja akijinasibu wakati wa sherehe hiyo.
Akiahirisha sherehe hiyo iliyohusisha burudani za kila aina, mwanachama nguli wa timu ya Yanga Audax Kamugisha, amewaasa waliohudhuria sherehe hiyo kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho timu ya Yanga itakumbwa na mabadiliko yaliyoanzia kwenye benchi la ufundi mara baada ya kuondoka kwa kocha mkuu Nasreddine Nabi.
"Yanga ni taasisi kubwa zaidi ya Nabi, Nabi ameondoka lakini Yanga imebaki, ameondoka Fei Toto Yanga imebaki, hakuna sababu ya kuwa na hofu, viongozi wetu wako kazini na mambo mazuri yanakuja", amesema.
Ili kuthibitisha ukubwa ya timu ya Yanga, Kamugisha alitolea mfano wa mchezo wa fainali ya kombe la shirikisho la Azam ambapo pamoja na kukosekana kwa wachezaji muhimu akiwemo Mayele, timu ya Yanga iliibuka kidedea.
Katika hali inayoonesha kuwa wananchi wamejaa furaha, sherehe hiyo imefanyika katika kipindi kisichozidi mwezi mmoja tangu kufanyika kwa sherehe nyingine kama hiyo siku chache mara baada ya timu ya Yanga kutawazwa kuwa mabingwa wa ligi kuu ya NBC.