WABUNGE WASHAURIWA KUTOA ELIMU KWA WANANCHI KUEPUKA UPOTOSHAJI SUALA LA BANDARI

Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wameshauriwa kutumia muda huu ambao wako kwenye majimbo yao kuwaelimisha wananchi, ili kuepuka upotoshaji unaofanywa juu ya suala la Bandari.

Ushauri huo umetolewa leo na Wazee na Machifu ambao wameungana na Kamati ya Amani na maridhiano ya mkoa wa Shinyanga, kupitia tamko maalum ambalo wamelitoa kwenye Mkutano wao na waandishi wa Habari, uliofanyika hapa mjini Shinyanga.

Viongozi hao wamedai kuwa, kuna upotoshaji mkubwa kuhusu suala la mkataba wa Bandari ambao unafanywa na watu wenye nia ovu, hivyo wabunge wanapaswa kutumia muda huu ambao wako kwenye majimbo yao kuwaelimisha wananchi, ili waelewe sawasawa kuhusu mkataba huo na umuhimu wake.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa Kamati ya Amani na Maridhiano mkoa wa Shinyanga Sheikh Balilusa Khamis, amewataka Watanzania ikiwemo wanasiasa kutumia Lugha ya staha pale wanapotoa maoni yao, na kuacha kutumia fursa hiyo ambayo wamepewa na Serikali kueneza chuki na maneno ya uchochezi dhidi ya Serikali pamoja na kuwakashfu viongozi wa nchi akiwemo Rais, hali ambayo wameitaja inatishia umoja wa kitaifa.

Tamko hilo la Wazee, Machifu na Kamati ya Amani na maridhiano mkoa wa Shinyanga, linakuja huku kukiwa na mjadala mkubwa juu ya uwekezaji katika bandari ya Dar es salaam kupitia mkataba unaodaiwa kusainiwa kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya DP World kutoka Dubai, ambapo wengi wanaotoa hoja mbalimbali wanadai kwamba, hawapingi mkataba, bali wanachopinga ni baadhi ya vipengele vilivyomo ndani ya mkataba huo, ambavyo havina maslahi kwa taifa.

Wakati huo huo, Serikali kupitia viongozi mbalimbali akiwemo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, wamekuwa wakitolea ufafanuzi uwekezaji huo na kuondoa dhana kuwa upo kwa ajili ya kuuza raslimali za nchi, na badala yake umelenga kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa nchi, kupitia raslimali zilizopo kwa kuzingatia maslahi ya taifa.

Waziri mkuu Majaliwa pia amenukuliwa na vyombo vya habari akieleza kuwa, Serikali itazingatia maoni yanayotolewa na wadau mbalimbali ikiwemo wananchi juu ya suala hilo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Amani na maridhiano mkoa wa Shinyanga Sheikh Balilusa Khamis akisoma tamko kwa niaba ya wenzake,kushoto ni Mwenyekiti wa machifu mkoawa Shinyanga Chifu Kidola II Charles Njange

Wazee na machifu wakiwa kwenye Mkutano na Waandishi wa Habari

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post